MAMLAKA ya mawasiliano nchini(TCRA) imewataka watoa huduma wote wa maudhui kwa kutumia ‘Cable’(Cable Operators) kuhakikisha kuwa wanaondoa chaneli za maudhui yaliozuiliwa kwa mujibu wa sheria mpaka watakapo wasilisha mikataba ya makubaliano katika yao na watoa huduma wa Azam,Dstv,Zuku na Star times.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa TCRA,kanda ya ziwa, Mhandisi Francis Mihayo wakati alipokuwa akiongea na wamiliki wa ‘Cable’ kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa.
Mhandisi Mihayo alisema hivi karibuni mamlaka yao imekuwa ikipokea malalamiko juu ya ukiukwaji wa sheria ya haki miliki na haki shirikishi namba 7 ya mwaka 1999 kutoka kwa watoa huduma makampuni ya Azam,Dstv na Zuku.
Alisema TCRA inapenda kuwakumbusha watoa huduma kwa kutumia’Cable’ kutoa huduma zao kwa mujibu wa sheria.Alisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtoa huduma atakayekiuka sheria,kanuni,taratibu na masharti ya leseni yake.
Aliahidi Mamlaka yao itaendelea kutoa leseni na kusimamia sheria na kanuni kwa makampuni ya utangazaji wa Televisheni wanaotoa huduma ya matangazo kwa kutumia Teknolojia ya Digitali kwa njia ya sateliti(DVB_S) pamoja na mifumo ya kutumia mitambo iliyosimikiwa ardhini(Terrestrial Television Broadcasting-DVB-T).
Mmoja ya wamiliki wa ‘Cable TV’,Adeltus Lunyali alisema wanaiomba TCRA iwe inatoa mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kujua mabadiliko mbali mbali ya sheria za Hati miliki.Lunyali aliwaomba wamiliki ‘Cable TV’ kuonyesha maudhui yanayotakiwa na TCRA.