Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yatishia kusimamisha leseni za Dstv, Zuku

10727 Pic+tcra TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imesema inakusudia kusimamisha leseni za kampuni za Multichoice Tanzania Limited wamiliki wa king’amuzi cha DSTV na Simbanet Tanzania Limited inayomiliki Zuku kwa kukiuka masharti.

Tangazo la TCRA lililotolewa kwenye vyombo vya habari jana lilieleza Zuku na Dstv zimekuwa zikionyesha chaneli zilizopo kwenye orodha ya zile za bure kinyume cha matakwa ya leseni zao.

TCRA imetoa tangazo hilo siku chache baada ya lingine lililoeleza kusudio la kusimamisha leseni ya kampuni ya Starmedia inayomiliki king’amuzi cha Startimes kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni.

Julai 27, TCRA ilitoa tangazo kwa umma ikieleza nia ya kuzuia leseni ya Starmedia kwa madai ya kukiuka masharti kwa kutoonyesha chaneli za bure na kutolipa faini iliyotozwa.

Msemaji wa Starmedia, Juma Suluhu alisema kampuni hiyo ina ving’amuzi vya aina mbili; kimoja kinaonyesha chaneli za bure (FTA decoder) ambacho huuzwa Sh89,000 na kingine chaneli hizo huonekana baada ya kulipia (Pay TV Decoder) ambacho bei yake ni Sh45,000. Alisema ipo namna ya kubadilisha Pay TV Decoder kuifanya kuwa FTA kupitia mawakala kwa kulipia Sh44,000.

Tangazo la TCRA la jana lilieleza Simbanet na Multichoice haziruhusiwi kubeba na kuonyesha chaneli za televisheni zenye leseni za kutazamwa bila malipo kupitia ving’amzi vyao isipokuwa TBC1 pekee.

TCRA imewahi kuziamuru kampuni hizo kuacha kubeba na kuonyesha chaneli hizo kwa kuwa ni kinyume cha matakwa ya sheria na leseni walizopatiwa.

Chaneli ambazo zinapaswa kuonyeshwa bure kwa mujibu wa TCRA ni ambazo zinatumia mtambo wa ardhini kama TBC1, ITV, Channel Ten, Clouds na Startimes. Zinazotumia satelaiti ndizo za kulipia.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala aliliambia Mwananchi jana kuwa, lengo si kuadhibu bali kuzingatia utaratibu wa kisheria uliopo.

Ofisa Habari wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema walipoona tangazo hilo wameshangaa kwa kuwa kampuni hiyo na TCRA walikuwa na shauri katika Tume ya Ushindani kuhusu jambo hilohilo.

Zuku walipotafutwa kupitia mawasiliano yaliyopo kwenye tovuti, aliyepokea simu akijitambulisha kuwa mtoa huduma kwa wateja alisema suala hilo hawezi kulitolea ufafanuzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz