Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yaonya utapeli huduma za fedha

FEDHA WEB TCRA yaonya utapeli huduma za fedha

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati watumiaji wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu wakiongezeka kutoka milioni 47.2 June hadi kufikia milioni 51.3 Septemba mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewatahadharisha watumiaji hao kuepuka utapeli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21, 2023 katika uwanja wa Sheikh Amri Abed jijini hapa katika maonyesho ya tatu ya wiki ya huduma za kifedha, Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa TCRA, Semu Mwakyanjala amesema ongezeko la watumiaji huduma ni asilimia 8.7.

Hata hivyo, amesema bado kumekuwepo na watu wasio waaminifu wanaotumia mitandao ya simu kutapeli, huku akitoa wito kwa wananchi kuwa makini na watu wanaowapigia simu ama kuwatumia ujumbe wa kutaka fedha.

"TCRA inashauri watumiaji wa huduma za simu za kiganjani kuhakikisha taarifa wanazopokea za kuwataka kutuma fedha kujiridhisha kutoka kwenye kampuni husika, kabla ya kutuma fedha ili kujiepusha na matapeli," amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali imeweka usalama kwenye mifumo ya kifedha nchini ili kudhibiti baadhi ya watu wanaotumia mitandao kama kichaka cha uhalifu.

Kwa mujibu wa Mwakyanjala, Tanzania ni nchi ya pili kwa utoaji huduma bora za kifedha kati ya nchi 55 za Afrika.

Akizungumzia watumiaji wa laini amesema wameendelea kuongezeka ambapo hadi Septemba 2023 kulikuwa na laini za simu milioni 67.12 kutoka laini milioni 64.01 za Juni mwaka huu sawa na ongezeko la asilimia 4.86.

Amesema watumiaji wa intaneti wameendelea kuongezeka kwa asilimia 1.24 kutoka watumiaji zaidi ya 34.04 milioni Juni na kufikia zaidi ya 34.46 milioni Septemba mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live