Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yanadi vitalu vya intaneti ya 5G

Tca Pic TCRA yanadi vitalu vya intaneti ya 5G

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Kampuni za Vodacom na Airtel zimegawana vitalu vinne kila moja kati ya 11 vya intaneti vilivyonadishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuziwezesha kutoa intaneti ya 5G.

Hivi karibuni, TCRA ilinadisha masafa ya mawasiliano kwenye bendi za 700MHz, 2300MHz, 2600MHz na 3500MHz kwa watoa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti na kampuni nne kati ya tano zilizojitokeza zikashinda.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabir Bakari amesema mnada huo umeiingizia Serikali jumla ya dola 187.496 milioni za Marekani (Sh436.2 bilioni).

“Kulikuwa na watoa huduma watano walishiriki kwenye mnada huo uliokuwa na vitalu 11 vya masafa, wanne wameshinda. Kampuni za Vodacom na Airtel zimepata vinne kila moja, Tigo imepata vitalu viwili na Halotel kimoja,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa vitalu hivyo, alisema Vodacom italipa dola 63.22 milioni sawa na Sh146 bilioni huku Airtel ikitoa dola 60.1 milioni sawa na Sh139 bilioni wakati Tigo ni dola 34 milioni na Halotel dola 30.16 milioni ambazo ni Sh69 bilioni.

“Masafa hayo yanatarajiwa kuleta manufaa kwa Taifa ikiwamo kuendeleza miundombinu ya mawasiliano ya kasi ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijiti katika sekta zote ukiwamo uchumi wa bluu, uwezeshaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi na kupunguza gharama za huduma za mawasiliano,” alisema.

Manufaa mengine alisema ni kuboresha na kueneza huduma za mawasiliano hasa vijijini, kuendeleza na kuwezesha ubunifu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Mnada huo ni wa pili kufanywa na TCRA baada ya ule wa Juni 2018 uliowezesha mawasiliano ya kasi ya 4G yanayotolewa na kampuni za simu nchini.

Chanzo: mwanachidigital