Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA yaja na king’amuzi kimoja

94876 Pic+kingamuzi TCRA yaja na king’amuzi kimoja

Sun, 9 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miaka sita iliyopita, Tanzania ilishuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya matangazo, mifumo ya analogia ilizimwa rasmi na kuanzishwa kwa matangazo ya dijitali.

Katika hatua hiyo, vituo vya televisheni vililazimika kurekebisha mitambo yake ya kurushia matangazo ili kuendana na mabadiliko hayo na wamiliki walilazimika kutoa mamilioni ya fedha ili kupata vifaa hivyo.

Baadaye lilikuja zoezi la kuzizima simu ambazo hazina viwango na lilifanyika hivyo na maelfu ya simu zilizimwa na hivi karibuni kulikuwa na uzimaji wa mamilioni ya laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Hiyo ilikuwa ni hadithi fupi ya mabadiliko yaliyofanyika katika sekta ya mawasiliano katika kipindi cha chini ya muongo mmoja; mabadiliko bado yanaendelea.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba aliliambia gazeti hili jana kuwa kabla ya mwaka huu kuisha, mfumo wa ving’amuzi utabadilika na badala yake wateja wataweza kutumia king’amuzi kimoja kupata matangazo yoyote ya vituo vya televisheni.

Mteja hatalazimika kuwa na ving’amuzi (decorder) nyingi bali atalazimika kununua kadi ya kituo cha televisheni anachotaka na king’amuzi hicho kipya kitaweza kumpa matangazo hayo.

Pia Soma

Advertisement
“Siwezi kusema hili litafanyika mpaka lini, lakini kabla ya mwaka huu kwisha litakuwa limefanyika,” alisema mkurugenzi huyo.

“Hili jambo ni mchakato, lazima ushirikishe wadau na wao waridhie. Ukisema uliharakishe utaharibu soko.”

Alisema jambo hilo ni lazima lifanyike kwa kuwa linajibu changamoto za watu wengi ambao wamekuwa wakilalamika mrundikano wa ving’amuzi nyumbani kwao na walikuwa wanalazimika kufanya hivyo ili kupata chaneli nyingi za maudhui wanayoyataka.

“Tupo kwenye advanced stage (hatua ya juu) ya mchakato na hatua hii itaondoa kilio cha watu wengi waliokuwa wanataka chaneli zinazoonyeshwa bure (FTA) kwa kuwa akiwa na kadi ya kisumbusi ambacho kinaonyesha FTA akitaka anachomeka tu kama unavyoweza kubadilisha laini ya simu,” alisema Kilaba.

Aidha mkuu wa Kitengo cha Leseni wa TCRA, Andrew Kisaka alisema mabadiliko hayo hayafanani sana na yale ya kutoka analogia kwenda dijitali kwa kuwa yanahusu upokeaji tu tofauti na awali wakati mabadiliko yalipohusu hadi mitambo ya kurushia matangazo.

Alisema kwa ving’amuzi, ambavyo pia vinaitwa visimbusi, itakuwa ni lazima lakini kwa TV ambazo zina uwezo wa kunasa chaneli litakuwa ni jambo la hiari.

Kisaka alisema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya kuwa na visimbusi vingi majumbani na shida inakuwa wakati mteja anapohitaji vipindi tofauti ambavyo vinapatikana katika visimbusi tofauti.

“Watu wamekuwa wanahangaika huku na kule unakuta visimbusi vingine anavitumia kwa muda mfupi tu wakati mwingine mtu anatamani angeweza kukinunua kwa muda fulani tu,” alisema.

“Na tatizo hilo si la kwetu tu tayari lilishazitesa nchi za Ulaya ndipo wakaja na suluhisho la namna hiyo.”

Alisema kwa kutumia teknolojia ya CAM mtu atakuwa na kisimbusi kimoja, lakini anakuwa na kadi za kielektroniki za watoa huduma tofauti ambao akiweka anapata huduma zao hivyo hivi sasa watoa huduma watakuwa wanauza CAM na sio visimbusi.

Chanzo: mwananchi.co.tz