Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCRA kutoa leseni kidijitali nyanda za juu kusini

Tcraaaaaaaaa TCRA kutoa leseni kidijitali nyanda za juu kusini

Mon, 4 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbeya. Ili kurahisisha huduma za mawasiliano Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) imetekeleza kampeni maalumu inayowawezesha waombaji wapya wa leseni za mawasiliano kuzipata kupitia mtandao.

Meneja wa mamlaka hiyo Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Asajile John amesema lengo la kampeni hiyo iitwayo leseni kidijitali ni kuongeza uelewa wa wadau wa sekta ya mawasiliano wanaotoa huduma za mawasiliano kupata leseni kwa haraka ili wananchi wengi zaidi waweze kuhudumiwa.

Mbali na kuongeza uelewa kwa watoa huduma za mawasiliano pia mamlaka hiyo imetoa elimu kupitia vyombo vya habari katika mikoa ya nyanda za juu kusini ili kuwafikia wananchi ambao ni watumiaji wa mwisho wa huduma za mawasiliano ili kuhakikisha wanatumia huduma zilizosajiliwa na TCRA.

“Mamlaka inatoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwamo ya vyombo vya habari katika kanda yetu yenye Mikoa saba ikiwa ni Mbeya, Iringa, Rukwa, Ruvuma, Katavi, Njombe na Songwe lakini ni muhimu kutimia huduma zilizosajiliwa," amesema

amezitaja leseni ambazo zinatakiwa kuombwa kwa njia ya kidijitali kuwa ni usafirishaji wa vipeto na vifurushi, maudhui ya habari na matukio mtandaoni, kuagiza na kusambaza vifaa vya mawasiliano, wasimikaji na wanaokarabati vifaa ‘mafundi simu’.

"Kwa sasa mwombaji wa leseni hahitaji kutembelea ofisi zetu ili kupata leseni, anaweza akaomba akiwa popote, tumefanya hivyo ili kuwarahisishia wateja wetu na mchakato huu umekuwa rahisi sana na yeyote anaweza akautumia mfumo huu,” ameongeza.

Amewataka watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha wanakuwa na leseni zinazowaruhusu kutoa huduma hizo na kwamba bila kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria ya mawasiliano ya kielektroniki na posta.

Ofisa Mawasiliano wa TCRA, Robin Ulikaye amewataka wananchi kuwatumia watoa huduma waliosajiliwa ili kulinda haki zao akisema mamlaka hiyo imekuwa ikiboresha huduma zake kulingana na mabadiliko ya teknolojia wameboresha mifumo ikiwamo kupokea changamoto za watumiaji.

“Njia ya kuthibitisha uhalali wa leseni ya mtoa huduma uliyochagua ni rahisi sana na ni kwa kutumia simu ya mkononi na kupata utaratibu wote kwa kuhakiki baada ya kuweka namba ya leseni kwa kutumia namba ya huduma za serikali unaweza kuthibitisha uhalali wa leseni,” amesisitiza.

Ulikaye amewataka wanaojihusisha uandaaji na uwasilishaji wa habari na matukio kwa njia ya mtandao kuhakikisha wanasajili televisheni,redio na blogu zao za mtandaoni na kuwataka mafundi simu kujisajili ili kupatiwa mafunzo na leseni.

Mmoja wa wananchi jijini Mbeya, Hadija Mhadhir amesema uwapo wa kampeni hiyo utaondoa usumbufu katika maombi ya leseni huku akiishauri mamlaka hiyo kuboresha sehemu ya mtandao ili kuondokana na kuchelewa kwa huduma.

“Hiyo ni mbinu nzuri ili kuondoa msongamano ofisi, lakini hata hivyo vitu vya mtandaoni muda mwingine huwa na changamoto za kupatikana huduma haraka kwa sababu ya mtandao huohuo, hivyo waboreshe kitengo hicho,” amesema Hadija.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live