Benki ya Biashara Tanzania (TCB), imetiliana saini ya makubaliano na Benki ya Letshego Tanzania, zikiwa na lengo la kuwaunganisha wateja wa Letshego kupata huduma kupitia benki ya TCB.
Hafla ya kutiliana saini, kati ya benki hizo mbili, ilifanyika jana Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa benki hizo.
Akizungumza kuhusiana na kutiwa saini kwa benki hizo, zikiwa na lengo la kuwaunganisha wateja wao kupata huduma pamoja.
Mkurugenzi wa Tehama na Oparesheni TCB, Jema Msuya alisema, wao kama TCB wameamua kuingia mkataba na Benki ya Letshego, ambapo kwa sasa wateja wa Letshego wataweza kuweka pesa kupitia benki ya TCB na moja kwa moja kuziona kwenye akaunti zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Letshego, Omary Mdangi, alisema, wameamua kuingia mkataba na Benki ya TCB kwa kuwa Benki hiyo imeonekana kuwa na Matawi mengi nchini ambayo ni Matawi 82 tofauti na Letshego ambayo yapo nane.
Aliongeza kuwa, hivi sasa wateja wote wa Letshego, mahali popote watakapo kuwa wataweza kuweka hela katika Tawi lolote la TCB au Wakala na moja kwa moja ikaonekana katika akaunti yake.
"Kwanzia sasa Mteja yoyote wa Letshego...asihofu kwa kudhani kuwa pengine hapo alipo hakuna Tawi au Wakala wa Letshego, anende kwenye Tawi lolote au Wakala wa TCB akaweke hela yake na moja kwa moja ataiona kwenye akaunti yake.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Letshego, Simon Jengojengo, alielezea kwa ufupi historia ya Benki ya Letshego na maana ya neno hilo.
"Kwanza kabisa Letshego ni benki ya Nchini Botswana na ilianzishwa mwaka 2016, ikiwa na lengo la kusaidia kwa kuwainua wafanyabiasha kukuza mitaji yao na maana ya neno Letshego ni Twende Pamoja!" Alisema Jengojengo.