Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCB kuongeza uzalishaji wa kahawa

Uzalishajipiic Data TCB kuongeza uzalishaji wa kahawa

Sun, 2 Oct 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), imesema imejipanga kuongeza uzalishaji wenye tija wa zao la kahawa hapa nchini kutoka tani 70,000 hadi kufikia tani 300,000 ifikapo mwaka 2025.

Hayo yamesemwa jana Oktoba Mosi, 2022 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Primus Kimaryo wakati wa kufungua tamasha la kahawa lililofanyika katika kiwanda cha kukoboa kahawa (TCCCo) kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

"Zao hili la kahawa ni la kimkakati na mkakati uliopo hivi sasa ni kuongeza uzalisha wa kahawa baada ya uzalishaji wa kahawa kupungua, hivyo tunachokifanya sasa kwa kushirikiana na wadau ni kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 70,000  hadi kufikia tani  300,000 nchi nzima".

Amesema wakati kiwanda hicho cha kukoboa kahawa kilipoanzishwa mpaka kufikia mwaka 1975 mkoa wa Kilimanjaro pekee ulikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 25,000 za kahawa na baada ya uzalishaji kupungua mkoa uliweza kuzalisha tani 3,000 pekee.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa zao hilo, Kessy Mashilano ameishauri serikali kuongeza maofisa ugani wa kutosha katika sekta hiyo ya kahawa ili kuondoa changamoto zilizopo kwa wakulima.

"Mpango wa Taifa uliopo ni kwamba ifikapo mwaka 2025 tuweze kuzalisha tani 300,000 za kahawa lakini hivi sasa tunazalisha kwa asilimia 25 utaona jinsi hili pengo lilivyo kubwa kwa miaka hii ambayo iko mbele yetu".

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda amesema zao la kahawa lina umuhimu mkubwa kwa Taifa kwani limekuwa likiliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni ambapo linachangia wastani wa asilimia 5 ya thamani ya mauzo yake.

"Kuporomoka kwa uzalishaji wa kahawa hapa nchini kumesababishwa na sababu mbalimbali hivyo kusababisha kuyumba kwa ufanisi wa uzalishaji katika kilimo cha kahawa na umeleta madhara makubwa katika vita yetu ya kuondoa umaskini mkoani kwetu na pia kuathiri uchumi".

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB, Praygod Godwin amesema benki hiyo kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa imejipanga kutoa mkopo wenye riba nafuu Sh84 bilioni kwa wakulima wa kahawa pamoja na vyama vingine mkoani Kilimanjaro  ili kuendelea kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz