Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetakiwa kuongeza mashirika yatakayotoa huduma ya usafir wa anga, ili kuleta ushindani na kupunguza gharama.
Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatano Novemba 22, 2023 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alipotembelea ofisi za mamlaka hiyo jijini hapa, huku akiitaka TCAA kusimamia miradi inayoendelea kutekelezwa, kwa kuzingatia ubora, muda pamoja na thamani halisi ya fedha.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, endapo idadi ya mashirika yanayotoka huduma za usafiri wa anga nchini yataongezeka, ushindani wa kibiashara pia utakuwa jambo litakalosababisha gharama za otoaji huduma hiyo kuwa nafuu.
"Tunayo mashirika zaidi ya 32 yanayotoka huduma nchini, lakini ukiangalia mazingira ya viwanja vyetu ni salama wito kwa TCAA ni kuangalia namna gani ya kuongeza mashirika haya ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kuvutia wawekezaji," amesema.
Aidha Kihenzile amesema: "Pia hakikisheni mnasimamia vyema mashirika hayo ili kudhibiti ajali na malalamiko ya abiria kwenye kusitisha safari, sambamba na miradi ikiwemo ujenzi wa chuo, ambacho ni miongoni mwa vyuo bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TCAA, Hamza Johari amesema miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa ikiwemo ile ya kubadilisha mfumo wa sauti inatarajiwa kukamilika kwa wakati.
“Maagizo yaliyotolewa na Serikali tutahakikisha yanatekelezwa kwa wakati na kwa ubora, likiwamo hili suala la kuongeza mashirika ya ndege ili kuongeza ushindani. Ushindani unapokuwa mkubwa hata gharama za usafiri zinapungua," amesema Johari.