Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TCAA yaanza kufunga rada mpya katika viwanja vyake

28323 TCAA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeanza kufunga rada mpya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

Kwa sasa, Tanzania ina rada moja ya kuongozea ndege iliyonunuliwa mwaka 2002 ambayo uwezo wake umepungua kutokana na kasi ya mabadiliko katika sekta ya usafiri wa anga.

Rada ya zamani ilinunuliwa kwa gharama ya Sh40 bilioni kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza lakini iliibua utata mkubwa baada ya kumhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Andrew Chenge baada ya kubainika bei hiyo ilikuwa kubwa kinyume na bei halisi.

Akizungumza jana baada ya kuwasili kwa mitambo ya rada hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema mradi wa ujenzi wa rada mpya nne utagharimu Sh67.3 bilioni na utachukua miezi 18 kukamilika.

Kampuni ya Thades ya Ufaransa ndiyo iliyoshinda tenda ya ufungaji wa rada nne mpya zitakazoiangaza Tanzania ambazo zitafungwa kwenye JNIA, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, Mbeya (Sia) na Uwanja wa Ndege Mwanza.

“Hizi rada zitafungwa kila moja kwa wakati wake. Hii ya Dar es Salaam inaanza kufungwa leo (jana) na itakamilika baada ya miezi mitano kuanzia sasa na ikikamilika inawashwa na itakayofuatia itakuwa vivyo hivyo hadi ikamilike yote minne,” alisema Johari.

Alitaja faida zitakazopatikana kutokana na mradi huo kuwa ni pamoja na kuiwezesha Tanzania kuboresha utoaji wa huduma za kuongoza ndege, kukuza sekta ya usafiri wa anga katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa zitawezesha pia ndege nyingi kupita katika anga la Tanzania kwa kuwa litakuwa salama zaidi.

Waziri wa zamani wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba wa mradi huo alisema, “Hivi sasa ndege zinazoruka urefu wa futi 24,500 anga la Tanzania hawazioni, rada za Kenya ndizo zinaziongoza, lakini hizi zikishafungwa hali hiyo itatengemaa.”



Chanzo: mwananchi.co.tz