Kuanzia Januari mwakani, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) itasimika mifumo mipya na ya kisasa ya mawasiliano ya sauti kati ya rubani na woangoza ndege katika baadhi ya viwanja vya ndege nchini.
Usimikaji wa mifumo hiyo mipya ya kimataifa ya redio za mawasiliano (VHF-Digital radio) unakwenda kuanza ikiwa ni zaidi ya miezi miwili tangu kupokelewa kwa vifaa vyake katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka nchini Norway na Italia.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi wakati Tanzania ilipoungana na nchi nyingine katika maadhimisho ya Siku ya Anga Duniani yanayoadhimishwa Desemba 7 ya kila mwaka.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa huduma za uongozaji ndege kutoka TCAA, Flora Mwanshinga amesema kufungwa kwa mitambo hiyo kutawafanya kuhama katika mifumo ya analogia kwenda dijitali.
“Mradi umeshaanza, lakini Januari mwakani mitambo hiyo itaanza kusimikwa na miezi mitano baadaye itakuwa tayari… itawezesha kuwepo kwa mawasiliano yaliyoboreshwa ya kidijitali,” amesema Flora.
Amesema maboresho hayo ni makubwa kuwahi kufanyika katika usafiri wa anga na yataboresha utoaji huduma za mawasiliano kwa watumaji wakuu wa anga la Tanzania ambao ni marubani.
Awali, alipozungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Teophory Mbilinyi amesema wakati wakiadhimisha siku hiyo wanakumbushana kuhakikisha kuwa anga la Tanzania na nchi jirani linakuwa salama kwa ajili ya watumiaji.
“Anga letu ni salama kwa sababu tuna mitambo na vifaa vya kutosha kuwasaidia marubani wanaopita katika anga letu, miaka mitatu iliyopita tuliunga rada nne kuhakikisha anga lote nchini linaonekana na tuna mitambo mizuri ya mawasiliano kati ya marubani na waongoza ndege.
“Kuwapo kwa maboresho hayo kuliifanya Tanzania kuibuka mshindi wa nne kati ya nchi za Afrika kupitia ukaguzi wa usalama katika usafiri wa anga,” amesema.
Wakati akipokea vifaa hivyo Oktoba mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema mifumo ya mawasiliano iliyopo imepitwa na wakati na ndiyo maana Serikali ilitoa Sh31.5 bilioni kununua mfumo mpya.
Alisema mitambo inahusisha redio za kidijitali za masafa ya juu, mitambo ya kurekodi mifumo ya mawasiliano ya sauti na mifumo ya kuunganisha na kuangalia mifumo ya mawasiliano.
“Ndege zinapotumia anga la Tanzania zitakapotaka mawasiliano popote pale zitakapokuwa zikiita tu, tunasikia kupitia mitambo hii, maana ni mfumo wa kitaalamu unaofanya kazi nchi nzima,” alisema Johari.
Alisema mifumo hiyo itafungwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Pemba, Uwanja wa Abeid Aman Karume Zanzibar, Songwe, Mwanza, Tabora, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Tanga na Mtwara.
Mbali na viwanja hivyo, pia mfumo huo utafungwa katika vituo 18 nchini ambavyo vimefanyiwa utafiti kwa lengo la kukuza na kurefusha mawasiliano ya sauti.
“Mfumo huu utachagiza idadi ya miruko ya ndege, pia mashirika ya ndege yanayokuja nchini pamoja na abiria,” alisema Hamza.