Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilshi Zanzibar imesifu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa jitihada inayofanya katika usimamizi wa sekta ya usafiri wa anga Tanzania bara na Zanzibar na kusababisha kuimarika usalama wa usafiri wa anga nchini.
Wajumbe wa kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake, Yahya Rashid Abdallah wametoa pongezi hizo wakati walipotembelea Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania wakiongozana na watendaji wa Mamalaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kwa ajili ya kujifunza na kuongeza uwezo wa kusimamia anga kwa njia za kisasa zenye usalama zaidi.
Akiupokea ujumbe huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Daniel Malanga amesema hata sasa wakati taifa linatimiza Miaka 60 ya Muungano, Mamlaka itaendelea kusimamia sekta hii muhimu kwa kufuata misingi na miongozo yote stahiki ya kitaifa na kimataifa ili Taifa liendelee kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta hii adhimu.
Wajumbe wa Baraza wamesema usalama wa anga unatakiwa kupewa kipaumbele na kutazamwa kwa upana wake katika kuimarisha huduma za uongozaji ndege ili kuiwezesha anga kuwa salama na kuleta tija.
Aidha wajumbe hao wameisisitiza TCAA kuhakikisha wakati wote inakua mstari wa mbele katika kupokea teknolojia mpya za sekta ya anga ili kuhakikisha taifa haliachwi nyuma na mageuzi yanayotokea kwa kasi duniani. -