Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBS yawafunza wauzaji mafuta ya kula 1,700

E68d5ae632fe98ece2d5c34a2b40990d TBS yawafunza wauzaji mafuta ya kula 1,700

Mon, 5 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewapa mafunzo wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa mafuta ya kula zaidi ya 1,700.

Mafunzo hayo yanahusu uzalishaji bora, uhifadhi sahihi wa bidhaa za mafuta hasa sehemu za kuuzia, ufungashaji sahihi na salama na umuhimu wa kuzingatia na kuweka taarifa sahihi na muhimu kwenye vifungashio.

Mafunzo hayo yametolewa na shirika hilo kwa wadau hao wa Kanda ya Kati kwa siku kumi katika maeneo ya Mkalama, Kiomboi, Sikonge, Urambo, Shelui, Manispaa ya Tabora na Nzega.

Maeneo mengine ni Igunga, Manispaa ya Singida, Kondoa Irangi, Kongwa, Mpwapwa, Kibaigwa, Chamwino, Itigi, Manyoni, Dodoma Jiji na Bahi.

TBS imetoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na maofisa biashara, afya na maendeleo wa wilaya.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajulisha wadau wa mafuta ya kula fursa zilizopo ndani ya serikali ili kuwawezesha kuboresha bidhaa zao, ziweze kukidhi matakwa ya viwango na kupanua wigo wa soko la ndani na nje ya nchi na kuwafanya kuongeza uzalishaji utakaopelekea kuinua uchumi wao.

Msasalaga aliwashauri wadau hao, kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu, ambayo itawalazimu kuteketeza gharama zao.

Meneja wa Utafiti na Mafunzo TBS, Hamis Mwanasala, alisema mafunzo hayo kwa wadau wa sekta ya mafuta ya kula, yataendeshwa katika mikoa yote nchini.

Kwa kuanzia yameendeshwa katika Kanda ya Kati, ikijumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.

“Mafunzo haya ni bure, serikali inagharamia kupitia TBS na tuna mpango wa kufikia wadau wa mafuta ya kula nchi nzima," alisisitiza.

TBS ilitumia pia mafunzo hayo kuelezea majukumu ya shirika ikiwa pamoja na yale yaliyokua yakifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati TBS, Salome Emmanuel aliwasisitiza wajasiriamali ambao bado bidhaa zao za mafuta hazijapatiwa nembo ya bora, kuchangamkia fursa ya bure kwa kutuma maombi ya kutumia alama ya ubora kupitia SIDO ili serikali iwatambue kama wajasiriamali wadogo na kati.

Mafunzo hayo yalihusisha wadau walioshiriki katika kumbi mbalimbali zilizoandaliwa na kutembelea maeneo yao ya uuzaji au uzalishaji kama vile Pandambili (Kongwa), Soko Kuu la Singida, Tarafa ya Pahi (Kondoa), Soko la Majengo (jijini Dodoma) na Mitundu (Itigi),

Mengine ni Soko Kuu la Nzega, Soko Kuu la Tabora na wauzaji wa barabarani waliopo Shelui.

Emmanuel alisema lengo ni kuwaelimisha juu ya madhara yanayotokea mafuta hayo yanapoanikwa juani, kwani mwanga, joto na hewa husababisha mafuta kuharibika kabla ya muda wa mwisho wa matumizi. Pia, husababisha madhara ya kiafya.

Kutokana na hali hiyo ,wadau walielekezwa kuboresha utunzaji kwa kuongeza kivuli cha vibanda vyao na kuweka taarifa za vifungashio.

Mzalishaji wa mafuta ya kula, Daud Makala na muuzaji wa Mafuta hayo, Eunice Maneno walioshiriki mafunzo hayo jijini Dodoma, walipongeza juhudi zinazofanywa na TBS kuwasaidia wadau wa sekta mbalimbali hususani mafuta ya kula kuzingatia viwango ili kuweza kupata masoko ndani na nje ya nchi na kuwa na ushindani huru sokoni.

Nao wauza mafuta ya kula katika masoko ya Singida na Tabora, waliiomba serikali kurahisisha upatikanaji wa vifungashio na kuhakikisha vinauzwa kwa bei nafuu, ili wajasiriamali nchini waweze kufungasha mafuta yao kwa vifungashio bora na salama, tofauti na sasa ambapo wanatumia zaidi vifungashio vilivyokwishatumiwa awali kwa bidhaaa nyingine.

Chanzo: habarileo.co.tz