Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kati limeteketeza kilo 4,056.596 za bidhaa za vyakula na vipodozi visivyokuwa na ubora, vyenye thamani ya Sh milioni 26.448.
Akizungumza baada ya kuteketeza bidhaa hizo, Ofisa Usalama wa Chakula TBS, Deus Deulle alisema bidhaa hizo zimepatikana kutoka kwenye maeneo ya biashara za maduka, maghala, baa, hoteli na stoo zilizopo katika halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma, Singida na Tabora, mikoa inayounda Kanda ya Kati ya TBS.
Bidhaa zilizoteketezwa zinajumuisha zilizogundulika kuwa zimeisha muda wake huku miongoni mwa hizo tarehe za mwisho wa matumizi zikiwa zimehaririwa na zile zilizogundulika kuwa na viambata vya sumu.
Deulle alisema bidhaa hizo zimekamatwa na shirika hilo kati ya Januari na Oktoba mwaka huu.
Alisema uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wake wa matumizi na zile zenye viambata sumu zinaathiri uchumi wa nchi pamoja na afya ya watumiaji.
Alisema bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimehaririwa zinaathiri upatikanaji wa virutubisho vinavyotegemewa, zinaweza kusababisha magonjwa ya muda mfupi na mrefu ikiwemo saratani.
Kwa upande wa vipodozi hasa vile viambata sumu, Deulle alisema athari zake ni za muda mfupi na mrefu ikiwemo kuathirika ngozi, macho, mfumo wa uzazi kwa akinamama, ukuaji kwa watoto na magonjwa ya saratani hasa ya ngozi.