Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa amelitaka Shirika la Viwango nchini (TBS) kutoa majibu ya sampuli ndani ya siku moja badala ya siku tatu hadi saba kwa sasa.
Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 30, 2019 wakati akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo.
Amesema mitaani kuna kero ya ucheleweshaji wa majibu ya sampuli zinazotumwa, kwamba takwimu alizonazo zinaonyesha ni siku tatu hadi saba au zaidi.
“Matamanio yangu ni kuona siku moja tu watu wanapata majibu yao. Sasa hivi tupo katika teknolojia tutoke kwenye siku tatu hadi saba kwa sababu TBS inategemewa na Watanzania hasa wafanyabiashara,” amesema Bashungwa.
Kuhusu wafanyabiashara wa nondo kulalamikia Wakala wa Vipimo (WMA), Bashungwa amesema atakutana na watendaji wa taasisi hiyo pamoja na TBS kwa ajili ya kuzungumza kwa kina kuhusu changamoto hiyo.
“WMA na TBS wote wapo chini ya wizara hii tutakaa na kuangalia yote yanayotakiwa ushirikiano kati yao ili kuondoa sintofahamu kwa umma. Lengo letu ni kuwawezesha wafanyabiashara si kuwasumbua,” amesema Bashungwa.
Pia Soma
- Mzee wa Mahakama hatiani kwa kuomba rushwa ya Sh120,000
- Wanaume Kigoma Tanzania wahamasika kufunga uzazi
- Makinda abanwa kwa maswali, asema NHIF ilikuwa shamba la bibi
Wamedai maofisa wa WMA wakienda kufanya ukaguzi kwenye maeneo yao na kubaini nondo zimeongezeka urefu, wanakataa na kuwaeleza kuwa si kiwango kinachohitajika kisha kuwatoza faini.
Mkurugenzi wa TBS, Dk Yusuf Ngenya amesema wataongeza juhudi ili kuhakikisha majibu ya sampuli yanatolewa kwa wakati kama waziri alivyoeleza.