Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBS: Wafanyabiashara lindeni afya za walaji

28fc307c864b86fda8d9928382a10517 TBS: Wafanyabiashara lindeni afya za walaji

Tue, 16 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara kulinda afya za walaji na kukidhi matakwa ya sheria kwa kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi vyao.

Ofisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema hayo katika Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaliyoanza Februari 07 hadi 13, mwaka huu jijini Arusha yakiwa yameandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Shirika hilo linashiriki maonesho hayo ili kutoa elimu ya viwango kwa wananchi, wajasiriamali, wafanyabiashara na wadau mbalimbali likisisitiza ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kukua kiuchumi.

"Tunatoa mwito kwa wanaofika kwenye maonesho na hata ambao hawakufika, kusajili bidhaa na majengo ya vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria ambayo imetokana na Mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019 ili kulinda afya za walaji," alisema Mtemvu.

Sheria hiyo ilirudisha majukumu ya usimamizi wa usalama na ubora wa vyakula na vipodozi kwa TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Dawa na Chakula Tanzania (TFDA).

"Kwa hiyo usajili wa bidhaa, majengo ya vyakula na vipodozi ni takwa la kisheria ili kuwawezesha kufanya biashara zao kwa urahisi," alisema Mtemvu wakati akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye maonesho hayo.

Alisema usajili majengo ya biashara unawapa wafanyabiashara uhakika wa kutunza bidhaa na kwamba wanasajili jengo kulingana na bidhaa zinazokusudiwa kuhifadhiwa humo.

Kuhusu usajili wa bidhaa, Mtemvu alisema eneo linalohusika ni bidhaa za chakula na vipodozi.

Alisema usajili wa vipodozi unalenga kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku katika soko la Tanzania haviingizwi nchini kutokana na kuwa na viambata sumu.

Wakati huo huo, Mtemvu ametoa mwito kwa wajasiriamali kujitokeza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao TBS na akweka bayana kuwa huduma za usajilibure kwa kuwa gharama hizo zinalipwa na serikali ili kuwawezesha kufanya biashara.

Alisema wanachotakiwa kuwa nacho wafanyabiashara katika usajili huo, ni barua ya utambulisho kutoka Shirika l Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) ili kuanza mchakato wafikapo TBS.

Chanzo: habarileo.co.tz