Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBA kujenga nyumba 100 za watumishi

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma.  Katika kukabiliana na upungufu wa nyumba za watumishi wa serikali wanaohamia jijini Dodoma, Wakala wa Majengo nchini (Tba) wameanza ujenzi wa nyumba 100 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni Jijini hapa.

Hayo yamebainishwa leo Septemba Mosi na Ofisa Milki wa TBA, Fred Mangula wakati akizungumza na gazeti hili kwenye maadhimisho ya wiki ya zimamoto yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa.

Mangula amesema kuwa TBA ina jumla ya ekari 600 za ardhi zilizopo Nzuguni ambazo wanatarajia kujenga nyumba kwa ajili ya kuwauzia na kuwapangisha watumishi wa umma wanaohamia Dodoma.

"Sisi kama wakala wa majengo wa serikali tumejipanga kutatua changamoto ya uhaba wa makazi kwa watumishi wa umma wanaohamia makao makuu Dodoma, na kwa kuanza tutajenga nyumba 100 eneo la Nzuguni kwa ajili ya watumishi wa umma," amesema Mangula.

Ameongeza kuwa siyo hapo tu bali hata katika eneo la Itega lililopo jijini hapa wana eneo la ardhi ambalo watajenga nyumba kwa ajili ya viongozi ambapo ujenzi wa nyumba hizo utaanza hivi karibuni.

Pia amesema TBA iko kwenye mchakato wa kujenga nyumba nyingi za bei nafuu kwa ajili ya kuziuza na kuzipangisha kwa watumishi wa umma.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa TBA, Edina John amesema kuwa katika ujenzi wa majengo wanazingatia miundombinu ambayo haitasababisha nyumba kushika moto hata kama utatokea.

"Kwa hiyo kwenye nyumba tunazojenga tunahakikisha kuwa tunaweka miundombinu ambayo itawezesha nyumba kutoshika moto hata kama utatokea, na hii tumeifanya kwenye majengo mengi ambayo tumeshayajenga na ndiyo maana hakuna kesi za moto katika majengo yetu,"amesema John.

Amesema mpaka sasa wakala huo umeshajenga majengo mengi nchini kwa kuwa ina rasilimali za kutosha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ikiwemo rasilimali fedha.

Naye Rachel Kyando ambaye ni mpangiliaji majengo kutoka TBA amesema kuwa wakala huo ndiyo wakala pekee wa serikali katika ujenzi ambao hutoa ajira kwa jamii inayozunguka miradi inayotekelezwa na wakala huo.

Amesema TBA inatekeleza miradi mingi ya ujenzi hapa nchini kwa hiyo huwa inatia ajira kwa jamii husika kwa kushiki katika ujenzi wa miradi hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz