Kwa wengi unapozungumzia Kifua Kikuu (TB) hudhani ni ugonjwa unaoathiri kifua na mapafu pekee. Lakini madaktari wanasema zipo aina mbili za TB.
TB huambukizwa kwa njia ya hewa na bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis. Ipo TB ya mapafu na TB inayoshambulia nje ya mapafu.
TB za nje ya mapafu ni pamoja na TB ya mifupa, moyo, tumbo, figo, ngozi, damu, TB ya ubongo na TB ya pingili za uti wa mgongo.
Kwa mgonjwa mwenye moja ya aina hizi za TB atakuwa na dalili zote za TB na dalili nyingine kwenye eneo husika.
Mfano mwenye TB ya tumbo, maji hujaa tumboni.
TB ya ubongo yenyewe huweza kusababisha kifafa, upofu hata kupungua kwa uzito kulingana na eneo la ubongo lililoathiriwa. TB hii hutibika lakini huacha kovu.
Dalili za TB ni pamoja na homa kali wakati wa usiku, kutokwa jasho sana na kulowesha kitanda, makohozi kuchanganyika na damu na kukohoa kwa wiki mbili au zaidi.