Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TASO waiangukia Serikali kurudishiwa viwanja

Taso Pc Data.png TASO waiangukia Serikali kurudishiwa viwanja

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Chama cha Wakulima Tanzania (TASO) kimeiomba Serikali iwarudishie viwanja vya maonyesho ya wakulima maarufu nanenane kwani ni haki ya wakulima.

Chama hicho kimesema viwanja vya maonyesho ya nanenane hivi sasa vinaendeshwa na mamlaka za mikoa kinyume na taratibu za uanzishwaji wake lakini baadhi wameanza kubadili umiliki wake.

Maonyesho ya wakulima (nanenane) yaliondolewa na Serikali mwaka jana baada ya aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa wakati huo Profesa Adolf Mkenda kusema hakukuwa na fedha za kugharamia badala yake akasema fedha zilizopangwa zinaelekezwa kwenye utoaji wa elimu kwa wakulima.

Katibu mkuu wa TASO, Herry Beji ametoa ombi hilo leo Jumamosi Februari 19, 2022 jijini Dodoma wakati akisoma tamko la kamati kuu taifa kwa wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa chama hicho uliojadili kuhusu viwanja hivyo.

Beji amesema Serikali ilichukua mamlaka ya chama hicho ya kuviendesha viwanja vya maonesho ya wakulima na imeshachukua jukumu la kuratibu kazi zote zilizokuwa zikifanywa na TASO jambo ambalo limeanza kuleta mkanganyiko.

Amesema kutokana na hali hiyo, TASO wameshindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na rasirimali zote ambazo chama kilikuwa kikitegemea kujiendesha kuwa chini ya mamlaka za mikoa.

Advertisement “Tunaomba Serikali kuturudishia viwanja vyetu ambavyo tulikuwa tunaviendesha sisi kama chama cha wakulima lakini iturudishie jukumu letu la kuendesha maonyesho ya wakulima nanene ambayo sisi ndiyo tunahaki nayo kwa mujibu wa taratibu ”amesema Beji

Ametaja baadhi ya viwanja hivyo ni kiwanja cha maonesho ya wakulima nanenane Nzuguni (Dodoma), Nanenane Morogoro, Mbeya, Arusha na Lindi.

Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini TASO, Said Amanzi amesema mwaka 2017 chama hicho kilipokonywa usajili kutokana na changamoto zilizokuwepo wakati huo ikiwemo kufutwa kwa Taso.

“Kwa wakati ule jukumu lilikuwa chini ya Serikali, lakini sasa chama tayari kimerudishiwa usajili na wenzetu wa mikoa hawataki kurudisha viwanja na wengine wameanza kubadiri hata umiliki wa viwanja, hivi tunakwenda wapi,”amehoji Amanzi

Amanzi amesema kutokana na hali hiyo ya kupokwa viwanja na mamlaka ya kuendesha shughuli zote za nanenane wamekosa nguvu za kukiendesha chama na kusaidia wakulima kufikia malengo yao.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz