Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TASAC yaingia makubaliano na kuboresha usafiri majini

TASAC.jpeg TASAC yaingia makubaliano na kuboresha usafiri majini

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shirika la Uwakala wa MeliTanzania (TASAC) limeingia makubaliano na Serikali ya Burundi na Congo kwa lengo la kuboresha usafiri salama wa vyombo na abiria majini.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kujitokeza kwa baadhi ya changamoto  kutoka kwa wafanyabiashara na wasafiri majini na hivyo kuweka makubaliano yatakayokuwa na dira ya kuepuka changamoto hizo yatakayosimamiwa na mamlaka ya usafirishaji majini kati ya nchi zote tatu.

Akizungumzia baadhi ya Makubaliano baada ya kikao cha pamoja na mabalozi wa nchi hizo na wafanyabiashara mkoani Kigoma  Kaimu Mkurugenzi wa Usalama, ulinzi na Utunzaji wa Mazingira TASAC, Selestine Mkenda, amesema meli zote za abiria zitatakiwa kuonyesha vyeti vinavyo onyesha uwezo wa kubeba abiria na viti vyote vya abiria lazima vifungwe  kwenye sakafu ya chombo.

"Taarifa zitakazo kuwa kwenye cheti zitatumika kukagua meli kutoka nchi husika, endapo meli haitakuwa na cheti haitaruhusiwa  kuondoka mpaka itakapopewa cheti kutoka nchini kwake, " amesema Mkenda.

Akibainisha moja ya changamoto Mkenda amesema kuwa ni uwepo wa visa kwa wafanyabiashara wanaopeleka biashara nchini Congo ambapo suluhu yake itapatikana punde  nchi hiyo itakapojiunga na umoja wa nchi za Africa Mashariki.

Naye Balozi mdogo wa Congo mjini Kigoma, Nsenga Gaspara amesema Makubaliano yaliyofikiwa yatasaidia kupunguza migogoro iliyopo na kusaidia katika ukuaji wa uchumi kwa nchi hizi zinazotegemeana.

Aidha Mwakilishi wa balozi wa Burundi Ininahazwe Albert amesema nchi itakayokiuka  makubaliano hayo waitwe ili kupewa utaratibu utakaosaidia wananchi kusafiri na kufanya biashara zao kwa usalama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live