Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARI yapania kuinua kilimo cha karanga

Karanga Ed TARI yapania kuinua kilimo cha karanga

Wed, 16 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Mratibu wa Programu ya Utafiti wa Mbegu za Mafuta nchini, Joseph Nzunda, aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima wa Karanga yaliyofanyika katika Kijiji cha Ipapa, Kata ya Ipunga, Mbozi mkoani Songwe.

Alisema mbali na kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, pia lengo la serikali ni kuongeza tija kwenye kilimo cha zao hilo ili kuinua kipato cha mkulima na serikali kwa kuongeza uzalishaji utakaoongeza mauzo ya karanga.

Pia alisema serikali inalenga kuboresha lishe kwa wananchi ili kukabiliana na tatizo la udumavu linaloikumba mikoa mbalimbali ikiwamo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inazalisha chakula kwa wingi lakini bado tatizo hilo liko juu kuliko kiwango cha kitaifa.

“Tunataka kuongeza tija kwa maana ya kwamba katika eneo dogo ulilonalo mkulima, utumie mbinu za kisasa kuzalisha. Utumie mbegu bora ambazo zimefanyiwa utafiti ili upate mazao mengi. Kwa sasa nchi yetu inakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta, sasa hii ni fursa kwetu wakulima wa karanga,” alisema Nzunda.

Aliwataka wananchi kutumia fursa ya uwapo wa watafiti kujifunza mbinu bora za kilimo ili waachane na kilimo cha mazoea ambacho huwapatia mazao ya kujikimu badala ya kuzalisha kibiashara.

Ofisa Utafiti wa Kituo cha TARI Naliendele, Athanas Minja, alisema tayari ugunduzi wa mbegu bora za karanga umeshafanyika kwa kuzingatia mazingira mbalimbali ya nchi kulingana na hali ya hewa na uwezo wa kuhimili visumbufu.

Alisema kwa sasa wamegundua mbegu zinazokomaa haraka kwa ajili ya kulimwa katika mikoa inayopata mvua za wastani ikiwamo mikoa ya Kanda ya Kati na kwamba mbegu hizo zinakomaa baada ya siku 90 mpaka 100.

Minja alisema baadhi ya mbegu ambazo zinachukua muda mrefu wanahamasisha zilimwe katika mikoa inayopata mvua nyingi ili zisiharibike kwa kushindwa kukaushwa vizuri wakati wa mvua.

“Hizi mbegu ni nzuri kwa sababu zinahilimi magonjwa na visumbufu vingine vya mimea, hivyo tunawashauri wakulima waachane na mbegu za kienyeji ambazo wamekuwa wakizitumia na watumie mbegu hizi bora ili waongeze tija,” alisema Minja.

Alisema katika utafiti mbalimbali waliofanya wamebaini kuwa mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo ardhi yake inafaa kwa kilimo cha karanga ndiyo maana wameongeza nguvu ya kuhamasisha wakulima.

Chanzo: ippmedia.com