Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARI waagizwa kuwezesha nchi kutoagiza mbegu nje

5f46b1745e30bf1faaec879b4d6d625a TARI waagizwa kuwezesha nchi kutoagiza mbegu nje

Mon, 10 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kuongeza uzalishaji wa mbegu za aina mbalimbali ili zisiagizwe tena nje ya nchi.

Majaliwa alisema hayo wakati alipotembelea banda la TARI katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea katika viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Alisema anaifahamu vizuri taasisi hiyo, watafiti wake na kazi wanazozifanya hivyo wanachopaswa kukifanya kila mwaka ni kuongeza mbegu za kutosha kwa wakulima.

"Mi nimewaona ninawafahamu vizuri. Ninafahamu kazi zenu nzuri, nilikuwa Naliendele Mtwara niliona mpaka maziwa ya korosho, nilijua maziwa ni ya ng'ombe tu nyie watu mnatisha sana.

"Muhimu zaidi kwenu ni kuhakikisha hii hatua ya tafiti ambazo mmekamilisha ziendelee msitoke tena nje ya nchi kuagiza kitu ambacho mnafanya kila mwaka ongezeni uzalishaji," alisema Majaliwa.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo alisema wanatumia maonesho hayo kuanzisha vituo mahiri vya usambazaji wa teknolojia kwani mpaka sasa vipo vinane nchini.

Alisema kuwa pia katika kila kitua cha usambazaji wa teknolojia wanahakikisha anakuwepo mtumishi ili aweze kusimamia.

"Lengo isiwe tunafunga nanenane na kubomoa kila kitu wakati watu wa ile hamasa ya kutaka kuendelea kujifunza na kupata hizo teknolojia wapo.

"Tunafanya vile kuhakikisha tunawafundisha mabwana shamba au maofisa ugani na wakulima ili wapate hizo teknolojia," alisema.

Alisema hata kampeni iliyopo Kituo cha Naliendele ya kula na kunywa korosho haitaishia hapo bali itaendelea na kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwenye mazao yote ya mkakati kuanzia afya ya udongo, mkonge, pamba, mazao ya mafuta yakiwemo chikichi na alizeti.

Alisema watafiti wamejipanga ili kilimo kiweze kumkomboa mkulima, tafiti zisibaki kwenye makabati bali ziwafikie wananchi ili ziwezi kubadili maisha ya mtanzania.

Chanzo: habarileo.co.tz