Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TARI: 40% ardhi Tanzania inafaa kilimo cha mkonge

6ade80a10df049cd019f4213d901b28b TARI: 40% ardhi Tanzania inafaa kilimo cha mkonge

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Mlingano mkoani Tanga, imesema zaidi ya asilimia 40 ya maeneo nchini yanafaa kwa kilimo cha mkonge.

Mkurugenzi wa TARI, Kituo cha Mlingano, Dk Catherine Senkoro alisema hayo yamebainika kutokana na tathmini iliyofanywa hivi karibuni.

Senkoro alisema maeneo yanayofaa kulima zao hilo ni Kanda ya Ziwa eneo la Bariadi pamoja na Mkoa wa Tanga unaozalisha mkonge kwa asilimia 60.

Maeneo mengine kwa mujibu wa Dk Senkoro ni Kanda ya Kaskazini katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha; Kanda ya Mashariki katika Mkoa wa Morogoro ambao ni wa pili kwa kilimo cha zao hilo; Kanda ya Kusini katika mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na Kanda ya Kati Mkoa wa Dodoma.

“Kuna maeneo waliacha kulima zao hilo hivyo serikali imesema yarudishe kilimo hicho kwani itaongeza uzalishaji kwa kutumia mbegu bora na safi kutoka kituo cha Mlingano,” alisema.

Ilifahamika kuwa, kituo cha Mlingano kinawajibika na zao la mkonge na kutoa teknolojia zenye tija katika zao hilo ili kunufaisha wakulima na taifa kwa jumla.

Kwa mujibu wa Dk Senkoro kupitia utafiti na teknolojia, wanatamani uzalishaji ufike tani tatu mpaka tano kwa hekta badala ya tani moja kama ilivyo sasa.

Alitoa mwito kwa watendaji wa wilaya na mikoa kuyajua maeneo ambayo zao hilo linastawi ili kuweka nguvu zaidi kuwezesha uzalishaji wenye tija zaidi kwa kutumia teknolojia ya kisasa na mbegu bora.

“Mlingano imezalisha mbegu ambazo zinafaa, zina uzazi mzuri, zina uwezo wa kustahimili na kuzaa muda mrefu mpaka miaka 15,” alisema na kuongeza kuwa, mkakati uliopo katika kituo hicho ni kufikia mbegu milioni tano kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo wa TARI- Mlingano alisema katika kipindi hiki Tanzania inapoelekea kwenye uchumi wa viwanda, ni wakati mwafaka wa kuwa na malighafi za kutosha zitakazoongeza tija katika uzalishaji.

Alishauri wakulima wa mkonge kulima kilimo mseto kwa miaka mitatu ya mwanzoni kwa kuwa kuna nafasi kubwa ili wapate chakula pamoja na kupunguza palizi.

“Tunapendekeza wapande mazao ambayo yatarutubisha udongo kama maharage na kunde,” alisema.

Dk Senkoro alisema serikali kupitia Wizara ya Kilimo tayari imeweka rasilimali ya kuzalisha hizo mbegu, hivyo uzalishaji wa mbegu ukiwa wa kutosha wakulima watapata kwa wakati unaotakiwa.

Alisema kituo hicho kina mpango wa kutoa elimu kwa wakulima, halmashauri na maofisa ugani kupitia idara ya kusambaza teknolojia.

Kwa kuanzia kwa mwaka huu wataelimisha maofisa ugani 400 na wakulima 500.

Chanzo: habarileo.co.tz