Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TANZANIA KURIDHIA UHURU BIASHARA AFRIKA

6bd5ab2e6f8df95e92aff60e6efe9ada.jpeg TANZANIA KURIDHIA UHURU BIASHARA AFRIKA

Wed, 26 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).

Mkataba huo tayari umesainiwa na mataifa 54 kati ya 55 barani Afrika.

Balozi Mulamula alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa kuadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika inayofanyika Mei 25 kila mwaka, ikiwa ndio siku ambayo umoja huo ulianzishwa mwaka 1963.

Alisema mkataba huo ulioanza kutekelezwa Januari Mosi mwaka huu, umeridhiwa na mataifa 37 kati ya 54 barani Afrika.

Aidha, Balozi Mulamula alisema Tanzania kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), imeendelea kushiriki majadilianoyote ya kuondolewa kwa ushuru wa bidhaa yaliyofikia asilimia 75, majadiliano ya uasili wa bidhaa yaliyofikia asilimia 86 na tayari imeshawasilisha mapendekezo yake.

“Hilo likikamilika bidhaa zetu zitaweza kufika katika nchi yoyote Afrika kwa urahisi zaidi na hatua hiyo itatusogeza zaidi kufikia lengo la kuimarisha uchumi wetu na wa Afrika kwa jumla,” alisema.

Alisema lengo kuu la mkataba huo ni kuimarisha na kukuza biashara kwa mataifa yote ya Afrika ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vyote vya kiuchumi vinavyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Afrika kiuchumi.

Kwa mujibu wa Balozi Mulamula, Tanzania itakaporidhia mkataba huo, itapata manufaa mengi ikiwa ni pamoja na kupata masoko mengi ya bidhaa mbalimbali za kilimo pamoja na bidhaa za viwandani zinazozalishwa ndani ya nchi.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Umoja wa Afrika mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu ya Umoja wa Afrika isemayo: “Sanaa, Utamaduni na Urithi: Njia za Kujenga Afrika Tuitakayo.”

Mulamula alisema kwa sasa Umoja wa Afrika umeridhishwa na hali ya demokrasia katika mataifa wanachama kwani imeimarika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Sasa kuna maendeleo kidogo maana matukio ya kupindua serikali yamepungua, chaguzi zimeimarika na kupunguza malalamiko kwa mataifa mengi hali inayochangia kudumisha amani na utulivu barani Afrika,” alisema.

Balozi wa Comoro nchini, Hamad Albadawi ambaye pia ni Mkuu wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, alisema historia ya Afrika haiwezi kukamilika bila kutaja Tanzania kutokana na kutekeleza jukumu kubwa la kusaidia ukombozi wa bara hilo.

Alisema kutokana na dhima ya Tanzania kiuchumi katika Bara la Afrika, kila nchi inataka iwe na uhusiano wa kiuchumi na kisiasa na Tanzania kwa sababu Afrika ni Tanzania na Tanzania ni Afrika.

“Hakuna nchi leo hii inayoweza kuizungumzia Afrika huru bila kutaja mchango wa Tanzania, hata nchi yangu ya Comoro tunaiona Tanzania kama mhimili mkuu wa uchumi wetu na siasa yetu, bila Tanzania tusingeweza kuwa na Comoro ya leo,” alisema.

Mwaka 2013 Afrika ilizindua dira yake ya maendeleo, Ajenda 2063 ikilenga kuiletea Afrika maendeleo, amani na mshikamano zaidi kwa muda wa miaka 50 mbele.

Miongoni mwa waasisi wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) unaojulikana sasa kama Umoja wa Afrika ni pamoja na Julius Nyerere.

Wengine walioshiriki katika mkutano wa kuundwa kwake Mjini Addis Ababa mwaka 1963 ni Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya, Milton Obote (Uganda), Kwame Nkurumah (Ghana), Haile Selassie (Ethiopia), Gamal Abdel Nasser (Misri), Ahmed Ben Bela (Algeria), Ahmed Sekou Toure (Guinea) na Kenneth Kaunda (Zambia).

Chanzo: www.habarileo.co.tz