Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TANROADS na kibano cha tathimini

Tanroad Pic Data TANROADS na kibano cha tathimini

Mon, 6 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanaofanyakazi kwenye mizani ya kupima uzito wa magari  kujitathimini katika utendaji wao.

Waziri Mbarawa amesema kumewepo na malalamiko kutoka kwa  wamiliki wa magari kutotendewa haki kwenye mizani mbalimbali hapa nchini.

Agizo hilo amelitoa jana Jumapili, Juni 5, 2022 wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mizani Kimokouwa iliyopo wilayani Longido mkoani Arusha ambapo amesema Serikali inajitahidi kuboresha miundombinu ya mizani lakini baadhi ya  wasimamizi wake hawatendi haki.

"Unakuta mtendaji kaomba rushwa Sh100,000 na yule mtu hana ffedha hizo anawekwa pembeni na kuandikiwa faini  na ukiletewa ile faini ukitizama na thamani ya gari unakuta gari ina thamani ya Sh10 milioni 10 lakini faini aliyoandikiwa ni Sh30 milioni ataitoa wapi?." Alihoji 

Waziri huyo amesisitiza waliopata fursa ya usimamizi huo kutenda haki kwani kwa kufanya hivyo malalamiko yatapungua, nawaomba Tanroads kujitafakari katika utendaji kazi wenu.

"Mizani hii kama tukiisimamia vizuri na watakaopata fursa ya kusimamia wakiwa makini itasaidia kupunguza sana changamoto," amesema Profesa Mbarawa.

Hata hivyo Profesa Mbarawa amesema kuna baadhi ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watumiaji wa vyombo vya usafiri ambavyo vinachangia kuharibu miundombinu ya barabara ni kuzidisha uzito,kumwaga mafuta kuziba mifereji ya maji na uegeshaji holela wa magari.

Katika hatua nyingine aliwataka wamiliki wa magari kuzingatia sheria za nchi ikiwemo sheria za barabara kuepuka kuzidisha mizigo kwenye magari ili kuepukana na faini zisizo za lazima.

Amesema katika kuzingatia utunzaji wa miundombinu ya barabarani hapa nchini, Serikali imezingatia kujenga vituo vya kupimia uzito wa mizigo iliyobebwa kwenye magari lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu wa barabara zetu na kupunguza ukarabati wa mara kwa mara kwani fedha ni nyingi hutumika.

"Miongoni mwa vitu vinavyoharibu barabara zetu ni umwagaji wa mafuta, uzibaji wa mitaro na uzidishaji wa mizigo kwenye magari hivyo nawaagiza Tanroads kutoa elimu kwa madereva juu ya utunzaji wa barabara zetu" amesema Mbarawa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema Wilaya ya Longido ni wilaya ya kimkakati katika Mkoa wa Arusha kutokana na kuwa eneo la uwekezaji na vyote vinavyofanyika ikiwemo miradi ya maendeleo vinaongeza thamani ya mkoa huo.

Amesema kuwa  eneo hilo lina vivutio vingi vya utalii hususani katika barabara ya kilomita 110 kutoka Makao Makuu ya wilaya hadi kufika katika eneo la ikolojia ya Ziwa Natron Kuna vitalu vingi vya Uwindaji.

Amesema baada ya Rais Samia kufanya ziara nchini Kenya ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara mpaka wa Namanga kibiashara umefunguka  hivyo wanapambana kuimarisha na kukuza uchumi wa nchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurdin Babu amesema  kupitia filamu ya Royal Tour idadi ya watalii kutoka nchi jirani inaongezeka hivyo ni vyema katika mji mdogo wa Namanga wakaweka taa za barabarani ili kusaidia kuongeza usalama.

Amesema kuwa kumekuwepo na watendaji wachache wa Tanroads wanaojihusisha na masuala ya rushwa katika utendaji kazi na hali hiyo husababisha kuwaandikia faini waliozidisha mzigo baada ya kushindwa kukubaliana kama ilivyo matarajio yake.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Rogatus Mativila amesema ujenzi wa mizani hiyo umegharimu Sh 14.7 bilioni hadi kukamilika kwake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live