Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TANAPA yaibua mkakati kabambe wa utalii

Tanapa Spokesperson Pascal Shelutete TANAPA yaibua mkakati kabambe wa utalii

Thu, 17 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Kamishna Uhifadhi Msaidizi Mwandamizi wa Mawasiliano wa TANAPA, Paschal Shelutete, alibainisha hayo jana kwenye semina iliyoandaliwa na shirika hilo kwa waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma.

Alisema shirika linatekeleza shughuli za uhifadhi na utalii kulingana na Mpango Mkakati wa miaka mitano (2018/19 – 2022/23) ambao  umefanyiwa marejeo na kuandaa mkakati mwingine wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/22-2025/26.

Shelutete alisema mkakati huo unalenga kutekeleza maagizo ya serikali katika sekta ya utalii nchini.

Alitaja eneo lingine litakalopewa kipaumbele kwenye mkakati huo ni kuimarisha miundombinu ya utalii hususani barabara, viwanja vya ndege, malango, magati, malazi, mawasiliano, maji na umeme.

“Pia kubuni na kuboresha utangazaji wa vivutio vya utalii kupitia televisheni ikiwamo Tanzania Safari Channel ya TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania), vipindi vya redio na mitandao ya kijamii,” alisema.

Kamishna huyo alisema shirika linatoa pia fursa kwa sekta binafsi katika kuendeleza na kukuza utalii katika hifadhi za taifa, kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi na umma ili kuwekeza katika maeneo ya hifadhi.

“Kuhamasisha jamii ili ijue umuhimu wa utalii na watalii wa ndani watembelee hifadhi za taifa na eneo la saba ni kuimarisha mikakati ya kudhibiti ujangili wa wanyamapori,” alisema.

Alisema katika miaka mitano hiyo ijayo shirika limejipanga kuongeza uwezo wa malazi kwenye hifadhi kutoka vitanda 3,429 hadi 5,000.

Akitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, Shelutete alisema ni uwekezaji wa puto katika hifadhi za Serengeti, Tarangire na Ruaha, utalii wa ‘canopy walkway’ katika Hifadhi ya Ziwa Manyara na Kitulo.

“Upembuzi unaoendelea wa kuwekeza katika utalii wa “cable cars” kutoka lango la Machame hadi uwanda wa Shira katika Hifadhi ya Kilimanjaro, pia uwekezaji kwenye miradi ya kimkakati ya kukuza utalii unaoendelea katika hifadhi za Rubondo, Burigi-Chato na Serengeti,” alisema.

Awali, akifungua semina hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Dodoma, Ahmed Mbugi , aliwashauri waandishi wa habari kutumia kalamu zao kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo  nchini ili kuhamasisha wananchi kufanya utalii wa ndani.

Aidha, Mbugi alisema baadhi ya wananchi wanaamini kuwa kutembelea vivutio vya utalii ni lazima waende hifadhi za taifa lakini katika Mkoa wa Dodoma na maeneo vipo vivutio ambavyo wananchi wanapaswa kutembelea na kujifunza historia mbalimbali ikiwamo kambi za wapigania uhuru.

Naye Ofisa Uhifadhi Mkuu wa shirika hilo, July Lyimo, alisema utalii husaidia kukuza uchumi na pato la taifa, kutambulisha nchi na kuongeza ajira huku akiwahimiza waandishi kuandika habari za kuhamasisha Watanzania kutembelea hifadhi na kujifunza mambo mbalimbali.

Chanzo: ippmedia.com