Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAMISEMI yataka ujenzi wa vitega uchumi

Tamisemi Uchumi TAMISEMI yataka ujenzi wa vitega uchumi

Sat, 12 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Katibu Mkuu Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Switbert Mkama ameyataka majiji na halmashauri zote nchini kuhakikisha zinajenga vitega uchumi vitakavyowezesha kuwaingizia mapato ikiwemo kuendana na kasi ya teknolojia.

Aidha, Jiji la Arusha limepongezwa kwa jinsi linavyotoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi mbalimbali vinavyozalisha bidhaa za viwandani ikiwemo vijana kujiajiri kupitia bodaboda.

Akitoa rai hiyo jana wakati wa ziara maalumu ya kukagua miradi ya Jiji hilo, Mkama alisema ili majiji na halmashauri yaendane na kasi ya teknolojia ni vema sasa kufikiria kujenga vitega uchumi kwa ajili ya kuwezesha mapato zaidi.

Alisema anataka kuona Jiji la Arusha linakuwa na miradi mbalimbali ya kiuchumi na kuleta taswira halisi ya Geneva ya Afrika ili hata pale serikali itakapofikiria kuleta miradi mbalimbali ya kimkakati maeneo yawepo ambayo yametengwa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo waliishukuru serikali kwa kuagiza kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia miradi waliyobuni ya kutengeneza PVC huku kikundi kingine kikinunua bodaboda 24.

Katibu wa Kikundi cha Maluile, Levina Shayo alishukuru Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) mkoani hapa kuwapa eneo ambalo wanakaribia kupaua ili kuweka kiwanda cha kutengeneza PVC.

Kwa upande wake Katibu wa Kikundi cha Ukombozi Bodaboda kilichopo Kata ya Ngarenaro, George Ernest alishukuru Jiji la Arusha kuwapa mkopo wa Sh milioni 60 kwa ajili ya kununua bajaji nane ila baada ya kupanda kwa bei za bajaji wakati mkopo ulipotoka waliomba kubadilisha mradi na kununua pikipiki 24 zinazoingiza Sh milioni 6.7 kwa mwezi na kushukuru kupata ajira za madereva ambapo ni vijana.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa jiji hilo, Dk John Pima alitoa rai kwa wanavikundi wanaochukua mikopo katika halmashauri hiyo kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili kutoa fursa ya vikundi vingine kukopa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live