Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAFIRI yapewa msaada vifaa vya utafiti

TAFIRI UTAFITI TAFIRI yapewa msaada vifaa vya utafiti

Thu, 13 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI ya Tanzania imepokea msaada wa vifaa vya utafiti wa maji baridi katika maziwa.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya dola 200,000 sawa na Sh milioni 460 vimekabidhiwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe ambaye ameshuhudia mkataba wa makabidhiano wa vifaa hivyo, pia amefungua mafunzo ya namna ya kutumia vifaa hivyo vya maabara kwa wataalamu wa utafiti TAFIRI.

Ameishukuru China kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kuhakikisha inatoa mafunzo yanayolenga kutoa ujuzi na wataalamu wa kutosha.

Amesema, China imekuwa ikiisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali na kwamba mafunzo hayo yanayohusiana na usalama wa maji baridi kwenye maziwa ya Victoria, Nyasa na Tanganyika.

“Mafunzo ya kubadilishana uzoeufu watafiti wetu wa Tanzania watapata kutoka kwa wenzao wa China, ushirikinao huu ulisainiwa 2008 kimsingi umesaidia katika mambo mbali mbali ya tafiti katika usalama wa maji na umesaidia wataaalamu wetu 10 kupata shahada za uzamili na uzamivu, ”amesema Prof. Shemdoe

Naye, Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania, Sue Peng amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kujenga uhusiano mzuri kati ya Tanzania na China.

Amesema, mafunzo yanayotolewa na China ni ya siku mbili, ambapo wataalamu wa Tanzania watafundishwa kuhusu matumizi ya vifaa vya kupima ubora wa maji baridi ambako samaki wanapatikana kwenye mazingiara ambayo maji ni safi, ikolojia ya usalama wa maji na uvuvi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dk Ishmael Kimirei amesema vifaa vya utafiti walivyopokea ni vya maabara ambapo ni Microscope, vifaa vya kwenda uwandani kwenye maziwa na bahari, CTD kwa ajili ya kupima hewa ndani ya maji, kina cha maji, joto la maji, hali ya acid na kuangalia vimelea kwenye maji ambapo awali hawakuwa nacho.

Amesema, vifaa walivyokuwa navyo awali ni vya kuchuja maji yanayotumika maabara, ambapo teknolojia iliyopo ni kuchemsha maji na kugandisha mvuke ndio upate maji safi kwa ajili ya kutumika kwenye maabara, lakini mara nyingi yanakuwa bado na tindikali ndani yake.

“Pia teknolojia hii inatumia umeme mkubwa sana, ili kupata maji hayo kwa ajili ya kusafisha vifaa na kuvitumia kwenye maabara, kwa hiyo vifaa hivi vipya tulivyoletewa vitapunguza gharama ya kusafisha maji na kutupunguzia majukumu ya kuchemsha maji, ”amesema.

Amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza gharama za kusafirisha sampuli nje ya nchi kwa ajili ya tafiti na kwa siku kuna sampuli zaidi ya 1,000 zinasafirishwa kwa ajili ya uchambuzi.

“Sampuli za maji na sampuli za udongo mara nyingi tunazopeleka nje ni ‘genetics’ na madini tembo sehemu nyingine hapa nchini kufanya analysis ni dola 10 kwa ‘parameter’ 1 sasa sampuli 10 ni dola 100,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live