Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yatoa bil 300/-miradi ya kilimo

20fe527377e8a0696707835d15533a4f TADB yatoa bil 300/-miradi ya kilimo

Sun, 21 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa zaidi ya Sh bilioni 300 katika sekta ya kilimo katika kipindi cha miezi 24 iliyopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine alisema hayo hivi karibuni wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro wakati wa ziara ya Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ya kukagua miradi ya umwagiliaji na hali ya uzalishaji sukari kwenye viwanda vya Kilombero , Mtibwa , Mkulazi II ambako alizungumza na wakulima wa miwa katika maeneo hayo.

Justine alisema kuwa kiasi hicho cha fedha, kimetolewa kwa kipindi hicho ajili ya kuwezesha miradi mbalimbali ya sekta ya kilimo nchini ikiwemo na uendelezaji wa zao la miwa na uanzishwaji wa viwanda.

“Nina furaha kubwa kujumuika na waziri kwenye ziara yake kwa ajili ya zao la sukari na pia naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano, kazi iliyofanyika ni kubwa “ alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TADB.

Justine alisema kutokana na ushirikiano na CRBD na Standard Chartered, benki yake imewekeza kwenye uzalishaji wa sukari Bagamoyo, kuhakikisha nchi inaondokana na uagizaji sukari nje.

Alisema kwa mwaka huu, ipo fursa kubwa kwa wawekezaji kufungua zaidi viwanda vya sukari. Alisema wanapaswa kuwasilisha andiko la miradi iweze kupitiwa na baadaye kupatiwa fedha za kuanzisha viwanda kulingana na maandiko yao vikiwemo vidogo vya wajasiliamali.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkenda aliwataka Watanzania na wawekezaji kutumia fursa ya mikopo ya benki katika kuanzisha viwanda hivyo.

"Nitoe rai kwa taasisi za kifedha za ndani kama TADB, CRDB, NMB na NBC watoe mikopo kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya sukari ili miwa ya wakulima ipate soko," alisema Waziri Mkenda.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Albinus Mgonya alisema sekta ya kilimo imechangia mapato ya halmashauri kwa asilimia 25.9 hadi 34 ambapo katika mwaka 2019/20 iliwezesha halmashauri kutoa mikopo ya Sh milioni 23 kwa vikundi 30 vinavyojishughulisha na kilimo.

Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeeland , alisema ili kuleta ushindani ni vyema serikali iruhusu ujenzi wa viwanda vingine vidogo kwenye eneo la viwanda vikubwa ili wakulima wachague eneo la kupeleka miwa yao, hatua ambayo italeta ushindani na suluhisho la matatizo ya wakulima.

Mmoja wa wakulima wa miwa , Seif Hassani kutoka Kijiji cha Mapambano wilayani humo, alisema licha ya kuzalisha miwa, mifugo imekuwa ikiwapa ikiharibu zao hilo shambani na kuwasababishia hasara, kwa kuwa kilimo wanachofanya kinatengemea fedha za mikopo.

Chanzo: habarileo.co.tz