Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yasaini mkataba kuwainua wakulima

Ee99340fe8a39d4b33d5ab070d11681e.jpeg TADB yasaini mkataba kuwainua wakulima

Fri, 27 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Kampuni ya Zana za Kilimo ya Agricom Afrika (AAL), wamesaini makubaliano ya kuwapatia wakulima matrekta na zana nyingine za kisasa za kilimo.

Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Derick Lugemala alisema jana Dar es Salaam kuwa ushirikiano huo ni wa kimkakati ili kuongeza idadi ya wakulima wanaotumia zana za kisasa walizozipata kwa gharama ndogo kupitia mikopo yenye riba nafuu.

“Hatuwezi tu kuwapa mikopo bila kuwashika mkono kwa kuwatafutia unafuu wakulima watoke kwenye kilimo cha mkono cha kujikimu na kuwekeza kwenye kilimo cha biashara,” alisema Lugemala.

Alisema ushirikiano wa TADB na Agricom utasaidia kuwapa wakulima fursa mbili za kipekee ikiwemo ya kupunguzwa riba kwa asilimia moja hadi nne na kupewa ruzuku ya hadi asilimia tatu katika gharama halisi ya kila zana itakayonunuliwa.

“Pamoja na hayo tuna riba maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana, ambapo mkulima anayeangukia katika kundi hili atalipia riba ya asilimia tisa, hii ni ahueni kubwa kwa wakulima wetu kwa sababu katika soko la kawaida la kibiashara, riba zinaweza kupanda hadi asilimia 18,” alisema Lugemala.

Alisema hadi sasa TADB imekopesha zana za kisasa 128 yakiwemo matrekta, mashine za kusaga na zana zingine.

Mwenyekiti wa Agricom, Angelina Ngalula alisema sababu kubwa ya kusaini randama ya makubaliano hayo ni kwa ajili ya kuchagiza ufumbuzi wa kibunifu katika ngazi zote za mnyororo wa biashara ya kilimo, kuongeza usalama wa chakula na kuinua maisha ya wakulima.

“Lengo letu ni kufanya mageuzi ya kilimo kwa Watanzania, kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo cha kibiashara kwa ajili ya maendeleo ya mkulima na maendeleo ya uchumi wa nchi,” alisema Ngalula.

Alisema randama hiyo ya makubaliano, Agricom watakopesha wakulima matrekta aina ya Suraj, mashine aina za Kubota kwa ajili ya kuvunia na zana zingine.

Chanzo: www.habarileo.co.tz