Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yaongeza tija, yazuia upotevu mazao

2f0e74eafdb427c2f6aea9366bcab4cb TADB ilianzishwa ili kujenga uwezo wa kifedha

Thu, 12 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imesema mikopo inayotolewa kwa wakulima imewawezesha kukabili changamoto ikiwamo kuzuia upotevu wa mazao unaojitokeza wakati wa kuhifadhi.

Mkurugenzi wa TADB Kanda ya Magharibi, Andrew Ezekiel alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji ya benki hiyo kwenye kongamano la biashara na uwekezaji kutoka nchi tano zinazozunguka Ziwa Tanganyika na Ukanda wa Maziwa Makuu.

Ezekiel alisema TADB ilianzishwa ili kujenga uwezo wa kifedha kugharamia taratibu za kilimo kwa wakulima wadogo wakue kwa kulima na kuzalisha kwa tija.

Alisema TADB imekuwa ikitoa mikopo kwa wakulima kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ili kuzuia upotevu wa mazao wakati wa kuhifadhiwa kabla hayajaenda sokoni.

“Moja ya kazi kubwa ambazo tumeshafanya ni kuzifanya taasisi nyingine za kibenki za biashara ziweze kuwakopesha wakulima ambapo jumla ya benki 15 zimeingia mkataba na TADB na kiasi cha shilingi bilioni 130 zimeshatolewa kwa benki hizo ziweze kutolewa mikopo kwa wakulima wadogo,” alisema.

Ofisa Biashara wa TADB Kanda ya Magharibi, Patrick Kapungu alisema ili kufikia malengo ya kuinua sekta ya kilimo kwa wakulima wadogo wa kanda hiyo, wametoa Sh bilioni tano kwenda kwa wakulima wadogo na mkopo huo umeanza kuleta mafanikio katika kukifanya kilimo kuwa na tija.

Alisema hadi sasa TADB imetoa mkopo kwa vyama 12 vya msingi vya mazao (AMCOS) mkoani Kigoma ambako kiasi cha Sh bilioni 3.8 kimeshatolewa kwa vikundi hivyo na zimeanza kufanya kazi.

“Kwa sasa benki yetu ipo kwenye mchakato wa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 2.9 kwa AMCOS tisa ili ziweze kutekeleza mipango yao ya kilimo na shughuli za uvuvi na kwamba kumekuwa na hamasa kubwa kwa wakulima mmoja mmoja, vikundi na taasisi kuomba mkopo kuendeleza shughuli zao za kilimo, uvuvi na ufugaji,” alieleza.

Mwanachama wa ushirika wa maharage kutoka Nyakitonto AMCOS ya Wilaya ya Kasulu, James Bella alisema mkopo waliopata umekuwa na manufaa kwao ikiwamo kupata soko la maharage kutoka Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (UN WFP).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live