Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yakopesha wakulima, wajasiriamali bil 69/-

F8f68f56c3dc04d37b04281c0a14acdd TADB yakopesha wakulima, wajasiriamali bil 69/-

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika miaka miwili imetoa mikopo ya sh bilioni 69.4 kwa wakulima na wajasiriamali zaidi ya 8,500 nchini.

Ofisa Mwandamizi wa benki hiyo, George Nyamrunda, alisema wakati wa maonesho ya nne ya mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kuwa, benki hiyo imetoa mikopo hiyo ili wananchi wajikomboe kiuchumi.

Nyamrunda alisema taasisi 10 za kifedha zikiwemo benki za CRDB, Benki ya Posta Tanzania (TPB) zinatoa mikopo kwa makundi hayo.

"Mfuko huu unachagiza mabenki mengine na taasisi nyingine za kifedha kwa lengo la kukopesha wakulima na wajasiriamali kwa riba nafuu kwani awali mabenki yalikuwa yakitoa mikopo ya asilimia 20-24 hadi kufikia asilimia 14-17"

Meneja Mikopo ya Kilimo Kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB), Lucas Mtewele, alitoa rai kwa wajasiriamali na wakulima kufika katika benki hiyo wapate mikopo nafuu wajikwamue kiuchumi.

Injinia Andrew Ako ambaye ni Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)Mkoa wa Arusha alitoa rai kwa watanzania kufungua viwanda mbalimbali ili waweze kuunganishiwa umeme na kuzalisha bidhaa kwani uchumi wa kati unaendana na fursa za viwanda.

Taasisi 25 za mifuko ya uwezeshaji, wajasiriamali kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Dodoma na maeneo mbalimbali wanashiriki.

Wakati anafungua maonesho hayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema tathmini za mara kwa mara zinazofanywa na serikali kuhusu utendaji wa mifuko na programu za serikali za uwezeshaji zinaonesha kuwa mifuko hiyo na programu hizo zimechangia kwa kiwango kikubwa jitihada za kukuza uchumi na kupunguza umasikini.

Alisema, sambamba na programu na mifuko hiyo, Halmashauri 185 Tanzania Bara zimetoa shillingi bilioni 93.3 kupitia mifuko ya uwezeshaji wa makundi maalumu ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Fedha hizo, zimewezesha upatikanji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi 32,553.

Chanzo: habarileo.co.tz