Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yajipanga kuatamia wanafunzi bora wa kilimo

Wadudu Dawa Kilimo TADB yajipanga kuatamia wanafunzi bora wa kilimo

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Serikali ikijipanga sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 hadi mwaka 2030, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema itaanza kuatamia wahitimu wa masomo ya kilimo vyuoni wanaofanya vizuri ili kuongeza tija na kuyafikia malengo ya Serikali.

Akiongea wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika utafiti wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Jumanne Novemba 21, 2023, Ofisa Rasilimali Watu Mkuu wa TADB, Jacqueline Minja amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali na kukuza sekta hiyo.

“Benki yetu itaandaa programu bora ya kuatamia vijana wataofanya vizuri, programu hiyo itakayokuwa ya miezi 24, italenga kutoa nafasi kwa wahitimu bora kuweza kupata nafasi ya kujifunza kazi kwa vitendo katika benki yetu.

“Pia tunatambua uwepo wa mikakati mbalimbali ya serikali kama vile sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo imetilia mkazo umuhimu wa kuweka mazingiza wezeshi kwa vijana kujihusisha na shughuli za kiuchumi, ikiwemo kilimo cha kisasa na kibiashara. Kwa kutambua hili, kwa kuanza, TADB imefika hapa na kutoa tuzo kwa wanafunzi bora mwaka huu,” amesema Jacqueline.

Licha ya hilo, TADB imewapongeza wahitimu bora wa chuo hicho kwa kuwapatia zawadi ya fedha taslimu Sh5 milioni.

Motisha hiyo ya fedha, imetolewa na TADB kama sehemu ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kupitia mpango mkakati wake mpya uliozinduliwa mwaka huu.

Akizungumza katika mahafali hayo, Kaimu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda ameishukuru TADB kwa kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri pamoja na mpango wake wa kuandaa programu maalum ya kuwaatamia wahitimu wa fani ya kilimo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live