Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yaja na bidhaa tatu kuboresha kilimo, mifugo uvuvi

TADB AFD.png TADB yaja na bidhaa tatu kuboresha kilimo, mifugo uvuvi

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, (TADB) imezindua Mpango Mkakati wa miaka mitano pamoja na bidhaa tatu mpya za kifedha zinazolenga kuboresha sekta hiyo nchini.

Bidhaa hizo ni mikopo ya jumla kwa taasisi na benki, mitaji ya kuchangia na dhamana za wateja wadogo, zikilenga kuwawezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kuendesha shughuli zao ambazo ni sehemu ya uchumi wa nchi.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa Mpango mkakati wa miaka mitano, (2023-2027) pamoja na bidhaa hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema TADB itazikopesha benki na taasisi hizo kwa masharti nafuu ambapo zitatumia rasilimali husika kukuza uwezo wao wa kutoa mikopo.

"Bidhaa ya pili ni mitaji ya kuchangia, ambayo TADB itashirikiana na benki na taasisi washirika kutoa mitaji kwa kundi hilo. Tatu ni dhamana za wateja wadogo zinazotewa kwa benki za kibiashara na taasisi za kifedha ili waweze kuwakopesha wakulima," amebainisha Nyabundege.

Amesema fedha hizo zinatokana na TADB kupitia Serikali kupokea mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Sh212 bilioni, kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ikiwa na lengo kuu la kuiongezea benki uwezo wa kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo.

Ili kuendana na azma ya serikali kukuza kilimo, Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya Kiserikali nchini Ufaransa mwaka 2022 alishuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo baina ya TADB na shirika hilo la Kifaransa AFD, kutoa mkopo huo.

Fedha hizo zitaelekezwa katika mpango wa kitaifa wa mageuzi na ukuaji wa kilimo ambao unatekelezwa kupitia mradi wa ‘TADB Agricultural Challenge Initiatives’.

“Mradi huu haswa unalenga kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wakulima na wawekezaji wadogo na wa kati katika kilimo, kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana na kuongeza fursa za ajira katika sekta ya kilimo.

"Vilevile kukuza na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa chakula na lishe bora nchini na kuchangia ukulima unaozingatia na kuhimili changamoto za mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.

Kadhalika Nyabundege amefafanua kuwa mpango mkakati wa miaka mitano unalenga kuleta chachu ya ongezeko la huduma za kifedha zinazotolewa na benki nyingine kwenda sekta ya kilimo.

Amesema, TADB itachangia ukuaji wa mnyororo ya ongezeko la thamani kwa kutumia fursa zilizopo ndani sekta ya kilimo ili kufanikisha uwekezaji zaidi katika miondombinu ya uzalishaji, mashine, uhifadhi wa mazao, uchakataji, huduma za kimkakati na biashara ya bidhaa.

Amesema, benki hiyo pia itazingatia kilimo cha kisasa kinachoendana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuandaa mikakati inayoshugulikia mabadiliko hayo na kuongeza uwezo wa wakulima kudhibiti changamoto za mabadiliko hayo.

"Kuhusu suala la kupanua wigo wa ushirikishwaji wa kifedha, TADB itaongeza idadi ya wanawake na vijana wanaojishugulisha na kilimo, ambapo kwa sasa asilimia 46 ya wanawake na 44 ya vijana wanajihusisha na kilimo.

"Mwisho, tunajidhatiti kukuza uwezo kwa kujenga uhusiano chanya, kukuza rasilimali ifedha kwa ajili ya kilimo, kupanua wigo wa huduma, kujenga uwezo wa uongozi, uadilifu.

Akimuwakilisha Waziri wa Fedha, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo anayehusika na Usimamizi wa Uchumi, Elijah Mwandumbya amesema Serikali inafahamu umuhimu wa kilimo kwa uchumi wa nchi na kuahidi kuendelea kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Amesema Wizara imewezesha benki hiyo kupata bajeti ya benki ya kilimo kupitia bajeti ya Serikali.

Pia, amesema Serikali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita imeipatia benki hiyo kiasi cha Sh 235 bilioni ili kuwakopesha wakulima.

“Mwaka 2022/23, Serikali imewekeza jumla ya Sh751.1 billioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 155.3 kutoka Sh294.1 bilioni ilizowekeza katika sekta ya kilimo mwaka uliopita. Ongezeko hili kubwa linadhihirisha wazi nia ya serikali kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo,” amesema

Chanzo: mwanachidigital