Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TADB yaidhinisha mil 455.5/- ujenzi kiwanda cha korosho

F98fce8b028f4ac923b93216c9c6127f TADB yaidhinisha mil 455.5/- ujenzi kiwanda cha korosho

Tue, 28 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imeidhinisha mkopo wa Sh 435,500,000 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kidogo cha kusindika korosho ili kuliongezea thamani zao hilo, kuongeza Pato la Taifa pamoja na kuinua kipato cha mkulima.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa mradi wa ubunifu katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho chini ya Taasisi ya Care Tanzania wilayani Mkinga jijini Tanga jana, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TADB, Jeremiah Mhada, alisema benki hiyo imeidhinisha mkopo huo ambao utatumika katika ujenzi wa majengo ya kiwanda hicho, ununuzi wa mashine na vifaa vingine vya kuendesha kiwanda hicho.

“Fedha hizo zitatoka kwa awamu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kiwanda na awamu ya pili, kufadhili wakulima wa korosho pembejeo zitakazowawezesha kuzalisha korosho kwa tija na kupata bei nzuri sokoni,” alisema.

Alisema fedha hizo pia zitasaidia kutengeneza ajira kupitia kazi za ujenzi wa majengo ya kiwanda, ununuzi wa korosho kutoka kwa wakulima wadogo wa viwanda vya Sigaya Limited.

Mhada alisema majukumu ya TADB ni kuhakikisha mageuzi yanafanyika katika sekta ya kilimo na kuwabadilisha kutoka kilimo cha mazoea na kufanya kilimo biashara ili waweze kupiga hatua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo na kuwaunganisha na masoko kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Duga.

“Uchakataji wa korosho hapa nchini utasaidia kuzalisha bidhaa nyingine kama mafuta kwa asilimia 15 ambayo hutumika kama dawa na matumzi ya viwandani jambo litakaloongeza thamani ya zao hilo nchini,” alisema.

Alisema kwa sasa mafuta ghafi ya korosho yanauzwa katika soko la Umoja wa Ulaya, Marekani, Japan na Korea na wasambazaji wakuu ni India na Brazil.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Duga, Said Tuwano aliishukuru TADB pamoja na wawekezaji waliowekeza katika wilaya hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Maulid Surumbu, aliwataka wadau wote kutekeleza majukumu yao kuhakikisha uzalishaji wa zao la korosho unaongezeka nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz