Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TABOA wataka tiketi kielektroniki zisogezwe mbele

E2243102ca96a0e8d66b441fc6ab2418 TABOA wataka tiketi kielektroniki zisogezwe mbele

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimeshindwa kuafikiana na taasisi za serikali kuhusu kuanza matumizi ya tiketi za kielektroniki kama ilivyoelekezwa na serikali.

Katika mkutano wa chama hicho uliofanyika Dar es Salaam juzi ambao pia uliishirikisha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC), baadhi ya wamiliki walilalamika masuala mbalimbali ambayo wanadai kuwa yanawaongezea mzigo katika utoaji huduma ya usafirishaji.

Akiwasilisha taarifa ya chama hicho katika mkutano huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Taboa, Joseph John aliyataja baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa kutolewa ufafanuzi na mamlaka hizo kuwa ni pamoja na tozo ya asilimia mbili ya gharama za uendeshaji wa mfumo ambao umewasilishwa na Latra licha ya wao kuwa na wazabuni wao waliokuwa tayari kufanya kazi hiyo kwa tozo ya asilimia 0.7 ya gharama ya tiketi.

Mengine ni malipo kupitia T-Pesa ambapo mmiliki wa basi atalazimika kuweka kiasi cha fedha kwenye mashine ya kukatia tiketi (POS) ili kuweza kukatika tiketi kwa abiria.

Pia jinsi mamlaka husika zilivyojipanga kufanya uwiano wa kisheria katika kuendesha mfumo huo ili isifike wakati wakapigwa faini mara mbili kwa kosa moja.

“Kwa taswira ya haraka tunazo mamlaka mbili na kila moja ina majukumu tofauti ya kisheria. TRA itamtaka mmiliki kuhakikisha anatoa risiti, halikadhalika Latra inamtaka mmiliki kutoa tiketi, hivyo tutakuwa na risiti na tiketi, ni vema tuwe na hoja zenye nguvu ili kuzishauri mamlaka kuzingatia haya,” alisema John.

Jambo jingine lililolalamikiwa na wamiliki hao wa mabasi ni kuhusu tozo ya asilimia 0.5 ya mauzo ya tiketi inayotozwa na Latra kupitia mfumo huo kwa madai kuwa inawezekana vipi kutozwa na mamlaka hiyo wakati haitoi huduma yoyote kwao kwa sababu jukumu lake ni kudhibiti vyombo vya usafiri tu.

Aidha walilalamikia kutoshirikishwa katika mchakato wa kupatikana kwa mzabuni atakayeendesha mfumo huo wa ukatishaji tiketi, pamoja na kutaka wamiliki wa basi kutozuiwa kupewa leseni kwa sababu hajajiunga na mfumo huo hadi hapo mwafaka utakapopatikana Kutokana na hali hiyo mkutano huo uliazimia kutomtambua mtoa huduma ya kukatisha tiketi aliyetafutwa na Latra, badala yake wataendelea kuwatambua wazabuni ambao waliwapata kupitia zabuni zilizofanyika mapema mwaka huu.

Pia waliazimia mashine za kutolea risiti za EFD ziruhusiwe kutumika kukatishia tiketi ikiwa mwafaka wa jambo hilo hautapatikana, kuitaka Latra ijitoe katika uendeshaji wa mfumo wa ukatishaji tiketi hizo kwa kuwa haihusiki kwa namna yoyote katika ukatishaji wa tiketi.

Badala yake jambo hilo liwe chini ya TRA, pamoja na kutaka kusogezwa mbele muda wa kuanza ukatishaji wa tiketi za kielektroniki ili kuwezesha wadau kupata elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya mfumo huo.

Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Barabara, Johansen Kahatano, alieleza kukubaliana na baadhi ya hoja hizo ikiwamo kuongeza muda ili kuruhusu kutolewa kwa elimu zaidi.

“Tutafuta nafasi na uongozi wenu ili tuone jinsi gani tunaweza kulifanya hili, tunawahakikishia kila mmoja tutamfikia. Kuhusu suala la kuzuia leseni kwa wasiojiunga na mfumo huu pia lisogezwe mbele,” alisema Kahatano.

Kuhusu tozo ya asilimia 0.5 alisema kuwa hilo ni hitaji la kisheria lililowekwa na Sheria ya Mamalaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini ya mwaka 2019.

Chanzo: habarileo.co.tz