Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TAA yatangaza mikakati ndege zitue Dodoma usiku

Atcl TAA yatangaza mikakati ndege zitue Dodoma usiku

Fri, 5 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imesema Kiwanja cha Ndege Dodoma kitaanza kutoa huduma za ndege kuruka na kutua kwa saa 24 kuanzia Septemba mwaka huu.

Mei Mosi, mwaka huu ndege ya Shirika la Ndege la Precision namba PW 602 ilishindwa kutua katika kiwanja hicho kwa sababu ilifika usiku.

Ndege hiyo iliamriwa irudi katika Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam ikatua salama.

Mkurugenzi Mkuu TAA, Mussa Mbura alisema mahitaji ya huduma za usafiri wa ndege Dodoma ni makubwa na awali walikua na mruko mmoja kwa safari za ndege ya abiria kwa siku.

“Tunapata miruko zaidi ya saba hadi nane kwa siku, awali ilikuwa ni mruko mmoja, changamoto ya kiwanja cha ndege cha Dodoma ni miundombinu yake ya taa za kuongozea ndege ila sasa serikali ilitoa fedha na fidia zimelipwa na kazi ya kufunga miundombinu ya taa inaendelea,” alisema.

Mbura alisema kwa sasa ndege haziwezi kutua usiku katika kiwanja hicho kwa sababu hakina miundombinu ya taa za kuongozea ndege.

Alisema mfumo wa taa za kuongozea ndege ulianza kufungwa Machi mwaka huu baada ya serikali kutoa Sh bilioni 12 kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wakiishi jirani na eneo la kiwanja hicho.

Mbura alisema kazi ya kuweka taa za kuongozea ndege imefikia asilimia 40 na sasa wanasubiri taa zinazotengenezwa Hispania.

“Katika majaribio ya kuziwasha tunaenda na timu ya wataalamu wetu kuzikagua kagua wakati wa kuziwasha na Mei 13 mara baada ya majaribio ya mwisho tutazisafirisha kuja Tanzania, ni mzigo mkubwa na mzito ni zaidi ya kontena mbili hizo taa,” alisema.

Mbura alisema kwa sasa kiwanja cha ndege Dodoma kinaruhusu ndege kuruka na kutua kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni kwa mujibu wa waraka uendeshaji uwanja huo NOTAM namba B 0027/23, B 0026/23, B0025/23, B0024/23 na B0023/23.

Aidha, alisema kiwanja hicho kinaendeshwa kwa kuangalia mawio na machweo ya jua kulingana na taarifa za usalama wa anga namba GEN 2.7-4 ya Januari 5, 2017 na ndege haziruhusiwi kuruka wala kutua baada ya saa 12:30 jioni.

Mbura alisema kiwanja cha Songwe kimeshawekwa taa na huduma sasa zinatolewa kwa saa 24, kiwanja cha Songea maboresho yanaendelea na hivi karibuni huduma zitatolewa saa 24.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live