Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sweden yapunguza uhaba wa fedha TASAF

Fedhapic Sweden yapunguza uhaba wa fedha TASAF

Fri, 17 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Sweden imeipa Tanzania msaada wa Sh bilioni 44.3 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya pili nchini ulio chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Fedha hizo zitasaidia kupunguza upungufu wa Sh bilioni 540 zinazohitajika kuendesha mradi huo. Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa msaada huo Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema fedha hizo zimetolewa na Umoja wa Ulaya (EU) na zinasimamiwa na Ubalozi wa Sweden.

Alisema mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya pili nchini unakabiliwa na upungufu wa fedha na kuwa EU wametambua umuhimu wa mpango huo na kutoa ufadhili wa fedha hizo kuwezesha mpango huo kutekelezwa. Alisema lengo la ufadhili huo ni kuwezesha mpango huo wa kuboresha hali za kiuchumi za wanawake kwa kufadhili familia maskini kuweza kupata fursa za kuongeza kipato na huduma za kiuchumi na kijamii.

“Ni dhahiri kuwa ukitaka kutekeleza uhifadhi wa jamii kikamilifu, ukiwekeza kwa wanawake unakuwa ni mkakati utakaofanikiwa, natumaini EU na wafadhili wengine wataongeza ufadhili zaidi siku zijazo ili kupunguza uhaba wa fedha kwa ajili ya kutekeleza programu hiyo,” alisema.

Alisema mbali na msaada wa jana, Serikali ya Sweden imekuwa ikisaidia utekelezaji wa mpango huo tangu awamu ya kwanza mwaka 2015 kwa kutoa dola za Marekani milioni 86 na kufuatiwa na dola za Marekani milioni 63. Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Kimaendeleo kutoka Ubalozi wa Sweden nchini, Sandra Diesel alisema lengo la msaada huo ni kusaidia kaya masikini hususani wanawake ili waweze kujikwamua na kukua kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alishukuru kwa msaada huo na kusema fedha hizo zitasaidia kupunguza uhaba wa Sh bilioni 540 kufanikisha awamu hiyo ya pili. Alisema utekelezaji wa mpango huo nchini kwa awamu ya kwanza na sasa ya pili umekuwa na manufaa kwa sababu kaya 150,000 zilizonufaika na mpango huo zimeonesha viwango vya kujitosheleza kuondoka kwenye umaskini uliokithiri.

“Mpango huu umekuwa na tija kwa wanufaika kielimu, kiafya, mfano mwaka jana zaidi ya wanafunzi 1,200 waliosoma kupitia ufadhili wa mradi ya Tasaf, wamefaulu na kudahiliwa kwenda vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na mwaka huu idadi tunategemea itaongezeka,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live