Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Suala la mikopo halmashauri kujumuisha wanaume latua Serikalini

Pesa Fedhaddd Suala la mikopo halmashauri kujumuisha wanaume latua Serikalini

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: Mwananchi

Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo amesema wameendelea kushauriana na Serikali ili ikiwezekana mikopo itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, itolewe pia kwa wanaume wenye umri wa kuanzia 36 hadi kufikia 50.

Tarimo amesema mikopo hiyo inatolewa kwa wale wenye umri wa chini ya miaka 35, hali ambayo imekuwa ikiwanyima fursa wale wenye umri wa kuanzia miaka 36 na kuendelea.

Ameyabainisha hayo jana Machi 5 wakati wa mkutano mkuu maalumu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, uliokuwa na lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha mwaka 2022/23, ambapo amesema wanaume wamekuwa na kilio cha kuomba mikopo hiyo.

“Wanaume wanasema kwa upande wa vijana wakifikisha miaka 35 hawakopeshwi tena, sasa wanaomba Serikali ilitazame hilo, ili nao waweze kukopeshwa hadi wanapofikia miaka 50,”amesema Tarimo.

Aidha Tarimo ameomba pia viongozi kuhamasisha wale wenye sifa kujitokeza kuomba mikopo hiyo na kuhakikisha wanairudisha kwa wakati, ili kuwezesha na wengine kukopa na kuanzisha miradi ya maendeleo.

“Hamasisheni watu wenye sifa wajitokeze kunufaika na mikopo hii inayotolewa na halmashauri, lakini pia wale waliokopa warejeshe kwa wakati, kwani kwa mwaka Manispaa hii kwa sasa tunakopesha Sh960 milioni, fedha hizi zinaingia kwenye mzunguko Moshi mjini na kuwezesha watu kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo amesema mikopo hiyo imeendelea kutolewa kikamilifu na kusema kuwa vijana bado wamekuwa nyuma katika kuchangamkia fursa hiyo.

“Kwa upande wa mikopo ya vikundi niwaombe tusiwe wazito, kwani vijana mnatuangusha, kina mama wanafanya vizuri lakini kwa vijana asilimia nne haitimii na haiwezekani kusema kwa sababu vijana hawajajitokeza ihamishiwe kwa wanawake.

“Tuhamasishe vijana huko mtaani wajitokeze kuunda vikundi, fedha zipo, Rais amesema tutoe fedha hizo na hazina riba, vijana waje kuchukua ili kuanzisha miradi ya maendeleo na kujikwamua kiuchumi”.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Patrick Boisafi amewataka wanachama wa chama hicho kushikamana na kuendelea kuyasemea yale yote yanayofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo kwenye jimbo hilo.

“Ndugu zangu tuwe wamoja na tusikubali mtu kutugawanya makundi, kwani uchaguzi hauko mbali, na tunapaswa kujipanga ili kuhakikisha tunashinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025,” amesema.

Chanzo: Mwananchi