Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Suala la Bombardier mikononi mwa wanasheria

86437 Pic+bombadier Suala la Bombardier mikononi mwa wanasheria

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema wakati wowote ndege ya Serikali aina ya Bombardier Q400 Dash 8, itawasili nchini ikitoa Canada inakoshikiliwa, hata hivyo hakufafanua ni lini.

Akizungumza jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Kamwele alisema hivi sasa shirika hilo linamiliki ndege saba zilizonunuliwa katika kipindi cha chini ya miaka minne na kuna nyingine nne zinakuja moja ikiwa ni aina ya Bombardier Q400 Dash 8 ambayo inatarajiwa kuwasili wakati wowote.

Waziri Kamwelwe alipoulizwa iwapo ndege hiyo inayotarajiwa kuwasili ni ile inayoshikiliwa nchini Canada kutokana na madai ya Mkulima Hermanus Steyn, na kama Serikali imeshaamua mbadala wa mahali pa kununua ndege tofauti na Bombardier ya Canada.

Alijibu kwa kuuliza swali, “Kuna ndege inashikiliwa Canada?”

Akaongeza, “Suala hilo vyombo vya kisheria vinalifanyia kazi, acha vifanye kazi tusiingilie sana hayo mambo, tusubiri ikija tuulizane.”

Aliahidi serikali itatoa taarifa kuhusu jambo hilo ambalo alisema kwa sasa kuna timu ya wataalamu inalishughulikia.

Aidha, Kamwelwe alisema ndege nyingine aina ya Bombardier Q400 Dash 8 itawasilu mwezi Juni mwakani na ndege mbili aina ya Airbus A220-300 zitawasili kati ya Juni na Julai 2021.

Ameipongeza bodi na menejimenti ya ATCL kwa kufanya kazi nzuri huku akisema ndiyo sababu bodi hiyo imeteuliwa kulisimamia tena shirika hilo kwa miaka mitatu ijayo isipokuwa mjumbe mmoja ambaye hakueleza kwanini yeye ameenguliwa.

“Nikupongeze wewe mwenyekiti pamoja na wajumbe kwa kuteuliwa kwenu, uteuzi wenu kwa mara nyingine ni ishara tosha ya kuwa mnauwezo mkubwa na serikali ya awamu ya tano ina imani na nyie,” alisema Kamwelwe.

Aliitaka bodi hiyo kulisimamia vyema shirika katika kutekeleza mpango makakati wake huku akisema endapo mpango huo utaonekana haufai wasisite kuubadilisha ili mradi kuendana na mazingira ya soko la ushindani.

Kamwele alisisitiza huduma kwa wateja zenye viwango bora na vya kimataifa huku akikumbusha kuwa siku za nyuma kulikuwa na kuahirishwa kwa safari au kuchelewa kwa ndege na abiria walikuwa hawapewi taarifa mbalimbali kama zile za kuchelewa na kuongeza alikuwa anapigiwa simu na watu hadi saa saba za usiku wakilalamika lakini ana matumaini suala hilo limekwisha kwa sasa.

Chanzo: mwananchi.co.tz