Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stika za TRA kwenye pombe ‘feki’ zaibua mazito

8940 Stika+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Serikali imeombwa kuchunguza namna wazalishaji wa pombe kali za bandia wanavyopata stempu au stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ombi hilo lilitolewa jana na wafanyabiashara pamoja na wateja wa pombe hizo kutokana na kukamatwa kwa shehena ya vileo bandia aina ya Konyagi na Highlife katika eneo la Msaranga mjini Moshi, Jumamosi iliyopita.

Katika nyumba moja kulikutwa chupa tupu za Highlife 2,400, chupa zisizo na nembo 230, vizibo vya chupa za Konyagi, lita 750 za spiriti na jiko la ‘Mchina’ linalotumika kufungasha pombe hizo.

Mbali na malighafi hizo na zingine zilizojazwa pombe, katika nyumba hiyo polisi na maofisa wa TRA walikuta stempu za mamlaka hiyo ambazo hubandikwa katika vileo hivyo zikionyesha kuwa uhalali wa malipo ya kodi.

Mfanyabiashara mkazi wa Shanty Town mjini Moshi, Chriss Martin alisema inashangaza stempu za TRA kukutwa katika kiwanda bubu cha kuzalisha pombe hizo, hivyo Serikali inapaswa kuchunguza.

“Njia pekee ya kujua hizi stempu zinatokaje TRA na nani alipewa na kama ni mfanyabiashara mwenye leseni alipewa, je alitoa taarifa kituo chochote cha polisi kuwa ziliibwa?” alihoji mfanyabiashara huyo.

“Hii si mara ya kwanza stempu hizo kukutwa kwenye viwanda bubu. Ni vyema umma ukajulishwa zinatolewaje na katika utaratibu gani maana hapa tunacheza na uhai wa watu.”

Martin alitaka wahusika washtakiwe kwa uhujumu uchumi kwa kuwa madhara ya kiafya kwa wateja ni makubwa.

Mfanyabiashara Jackson Mlinge alidai ni lazima wapo maofisa wa TRA wasio waaminifu ambao hushirikiana na wanamiliki viwanda hivyo bubu kutoa stempu hizo.

“Zile stempu zina serial number (namba za utambuzi) ni issue (suala) ndogo tu. Waziri alete tume na aanzie kwenye hiyo shehena tujue mchawi wetu ni nani. Tuseme imetosha kwa pombe feki,” alisema.

Mkurugenzi wa Baa ya Hugo Garden, Bosco Simba alitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Shirika la Viwango (TBS) kufanya ukaguzi wa kuzagaa kwa pombe hizo.

“Mimi naamini wananchi na sisi hatujatimiza wajibu wetu vizuri. Haiwezekani shughuli ya kuzalisha pombe hizi feki inafanyika kwenye nyumba halafu majirani msishuku jambo,” alisema Simba.

TRA kujichunguza

Akizungumza katika eneo la tukio, ofisa mwandamizi wa kodi kutoka TRA mkoani Kilimanjaro, Tilson Kabuje alisema mamlaka hiyo itachunguza kujua uhalali wa stempu zilizokamatwa.

“Ili kujua uhalali wake kunahitajika kufanywa uchunguzi kwa kuwa pombe zinazotengenezwa katika kiwanda hiki zina stika tayari, hivyo ni lazima tuchunguze kujua amezipataje,” alisema ofisa huyo.

“Tunapompa mtu stika tunakuwa tayari tumemsajili kama mlipa kodi wetu ambaye ana kiwanda kinachotengeneza kinywaji kinachofuata taratibu zote kwa maana amesajiliwa.

“Lakini pia tunapompa stempu zina taratibu zake ambapo anaomba kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja ana uwezo wa kuzalisha kiasi kadhaa na tutampa stempu kuendana na kiasi alichosema.”

Kabuje alisema inapotokea mtu hajapewa stempu kwa taratibu zinazokubalika na wakakutana anazo hali hiyo huichukulia kwamba ni wizi ameufanya kinyume cha taratibu ya Mamlaka ya Mapato.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, ofisi yao itashirikiana na polisi kuchunguza namna stika na stempu hizo zilivyopatikana kwa vile mtuhumiwa wa tukio hilo hatambuliwi na TRA.

RPC Kilimanjaro afunguka

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah aliyeongoza operesheni hiyo, alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho bubu kujisalimisha polisi kwa vile anajulikana.

“Popote alipo tunataka ajisalimishe polisi mwenyewe. Huyu bwana ana kichumba kimoja, lakini ni mtaalamu. Malighafi yake ni ‘spirit’ na anachanganya anavyojua mwenyewe,” alisema Issah.

“Tunahitaji kuchunguza malighafi anayapata wapi. Kuna hii inatumika kwa kupaka rangi lakini watu wanakunywa. Ni hatari na upo uwezekano wa watu Kilimanjaro kunywa Sumu.

Kukamatwa kwa pombe feki, ni mfulizo wa ukamataji wa viwanda hivyo, lakini wakazi wa Moshi wamekuwa wakihoji mashauri ya kadhia hiyo kumalizika kimya kimya na wakati mwingine bila kufika kortini.

Mwaka jana, TFDA wakishirikiana na polisi pamoja na TRA walikifunga kiwanda kimoja cha pombe kali katika eneo la Kiboroloni kwa madai ya kuzalisha pombe kali feki za kiwanda kingine kilichopo mkoani Shinyanga.

Chanzo: mwananchi.co.tz