Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stempu za kodi za kielektroniki zapaisha mapato

Fa79cf676d21ba27ddc79dfde9f6dd9f.png Stempu za kodi za kielektroniki zapaisha mapato

Sat, 26 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tangu kuanza kwa Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) Januari 15, 2019 makusanyo ya kodi nchini yameongezeka.

Aidha, kutokana na mfumo huo idadi ya wazalishaji wa bidhaa za sigara, vinywaji waliokuwa wanalipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeongezeka na kufika 307 ukilinganisha wazalishaji 57 wa hapo awali.

Taarifa hiyo ya mafanikio imetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mkutano wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na watendaji wa TRA uliofanyika jana Dar es Salaam kuzungumzia kuhusu ushirikishwaji wa wananchi katika kampeni za Hakiki Stempu na Kamata Wote.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, Kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani, Herbet Kabyemela alisema katika makusanyo ya kodi yameongezeko kwa asilimia 86.2 katika makusanyo ya Kodi ya Ushuru wa Bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika bidhaa za mvinyo na pombe kali zinazozalishwa nchini tangu kuanza mfumo wa ETS kwenye bidhaa hizo Januari 15, 2019.

“Ongezeko la asilimia 93 ya makusanyo ya Kodi ya Ushuru wa Bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa maji yanayofungashwa kwenye chupa yanayozalishwa nchini katika kipindi tangu kuanza kwa mfumo wa ETS kwenye bidhaa hizi mnamo Novemba Mosi, 2020,” alisema Kabyemela.

Aliongeza kuwa pia kumekuwa na ongezeko la asilimia 30 ya makusanyo ya Kodi ya Ushuru wa Bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika vinywaji laini vinavyozalishwa nchini katika kipindi tangu kuanza kwa mfumo huo kwenye bidhaa hizo Agosti Mosi, 2019.

Ongezeko jingine alilolitaja ni la asilimia 6.2 ya makusanyo katika Kodi ya Ushuru wa Bidhaa na VAT katika bidhaa za sigara zinazozalishwa nchini kwa kipindi kuanza kutumika kwa mfumo.

Kabyemela alilitaja eneo jingine ni ongezeko la asilimia tatu ya makusanyo ya Kodi ya Ushuru wa Bidhaa na VAT kwa bidhaa aina ya bia zinazozalishwa nchini katika kipindi tangu kuanza mfumo wa ETS kwenye bidhaa hizo tangu Januari 15, 2019.

Aliongeza kuwa baada ya uzinduzi rasmi wa kampeni ya Hakiki Stempu, Februari 14, mwaka huu jijini Mwanza, wananchi wameendelea kupakua programu tumizi na kujiridhisha ubora wa bidhaa kabla ya kuzitumia ambako kwa muda wa wiki moja pekee, wananchi 4,511 wamepakua programu tumizi ya Hakiki Stempu ikilinganishwa na wastani wa wananchi 200 waliokuwa wanapakua kwa mwezi.

Alisema programu hiyo ya Hakiki Stempu ni maalumu kwa ajili ya kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kulinda afya zao na wakati huo huo serikali ipate kodi halali kutokana na ushuru wa bidhaa unaotozwa katika bidhaa husika kupitia mfumo wa stempuni za kodi za kielektroniki.

Alifafanua kwamba kwa kupitia programu hiyo, mtumiaji anaweza kujiridhisha uhalali wa bidhaa kwa kupata taarifa kuwa bidhaa hiyo imezalishwa au imeingizwa nchini na nani, lini na wapi na kwa hatua hiyo mtumiaji atakuwa na uhakika kuwa na bidhaa hiyo itakuwa imepita katika mikono ya vyombo vingine vya serikali vya udhibiti wa ubora.

“Aidha, kwa kupitia Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS) kunaiwezesha serikali kukusanya kodi halali kwa uhakika kutokana na taarifa zinazopatikana moja kwa moja toka kwenye mfumo, kwa sababu mfumo huu unachakata taarifa na kuzisafirisha kwenda kwenye mifumo ya TRA pasipo kuingiliwa na binadamu,” alibainisha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live