Benki ya Stanbic imeanzisha huduma ya ‘Mpambanaji’ambayo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kutatua changamoto ya mitaji na masoko.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Aprili 27, 2023 na Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Biashara za Kibenki wa benki hiyo, Fred Max wakati wa kongamano lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Commmunications Limited (MCL) kwa lengo la kujadili namna ya kuwezesha biashara changa, za chini, ndogo na za kati (MSMEs) kukua haraka.
Kongamano hilo linafanyika katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki jijini Dar es Salaam limedhaminiwa na Benki ya CRDB, Kampuni ya usafirishaji ya DHL, Benki ya Stanbic, Ashton, Benki ya NMB, Clouds Media na Ukumbi wa mikutano wa Dome.
Katika kongamano hilo, Max amesema benki yake imeamua kutoa fursa hizo ili wajasiriamali wakue na kuongeza mchango wao katika kukuza uchumi wa Taifa.
Max ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo, amesema waliamua kuanzisha programu ya 'Mpambanaji' inayowezesha biashara zisizo rasmi ambazo ni nyingi na kuzipeleta kwenye taasisi za kifedha.
Amesema watatoa mkopo usio na dhamana wa hadi Sh50 milioni kwa wajasiriamali na watawatafutia soko nchini China kwa kuwaunganisha na wadau wasambazaji walioko nchini humo.