Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stakabadhi ghalani wawapatia wakulima bil 28/-

B55895580be1502e4764541cfb73bf4c Stakabadhi ghalani wawapatia wakulima bil 28/-

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MFUMO wa stakabadhi mazao ghalani katika Mkoa wa Ruvuma umewawezesha wakulima kupata zaidi ya Sh bilioni 28.

Akizungumza wakati anafungua mkutano wa wadau wa mazao ya ufuta, soya na mbaazi jana, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kiasi hicho cha fedha kimepatikana katika msimu wa masoko wa mwaka 2020/2021.

Ameyataja mazao yaliyouzwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani kupitia minada mbalimbali iliyofanyika katika wilaya za Songea, Tunduru na Namtumbo kuwa ni ufuta, soya na mbaazi.

Kwa mujibu wa Mndeme, zao la ufuta kilo 12,234,737 zilizouzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh bilioni 25, soya kilo 1,499,077 ziliuzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh bilioni moja na zao la mbaazi kilo 4,260,77 ziliuzwa na kuwaingizia wakulima zaidi ya Sh bilioni 2.585.

“Mfumo wa stakabadhi mazao ghalani umeonesha mafanikio makubwa katika mkoa wetu, hivyo tunafanya tathmini ya msimu wa masoko uliopita 2020/2021 na kuratibu maandalizi ya msimu wa masoko wa 2021/2022 ambapo ununuzi unatarajia kuanza Mei 2021,”alisema Mndeme.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa alisema mfumo huo umeziwezesha halmashauri kukusanya ushuru kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo kupitia zao la ufuta pekee zilikusanywa zaidi ya Sh milioni 954 za ushuru kwenye halmashauri.

Mafanikio mengine ya mfumo huo ameyataja kuwa ni kufufuliwa kwa vyama vingi vya ushirika, kuongeza ajira na umerahisisha ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya mapato ya serikali kuu.

Awali akitoa taarifa ya mazao ya ufuta, soya na mbaazi kwenye mkutano huo, Mrajisi Msaidizi wa Vyama Vya Ushirika mkoani Ruvuma, Bumi Masuba ameutaja uendeshaji wa masoko ya mazao hayo ulifanyika kupitia vyama vya msingi 44 mkoani Ruvuma na kuleta mafanikio makubwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz