Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stakabadhi ghalani kutumika mauzo ya choroko, soya, ufuta, dengu na mbaazi

3e4a0953896b19bc07eb225d9f2ba2be Stakabadhi ghalani kutumika mauzo ya choroko, soya, ufuta, dengu na mbaazi

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

S ERIKALI kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), imetoa muongozo wa biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani utakaotumiwa na wakulima mwaka 2021 ili kuuza mazao ya kibiashara kama choroko, soya, ufuta, mbaazi na dengu kwa lengo la kukuza kipato cha mkulima.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa juzi, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk Benson Ndiege alisema mfumo huo ni mzuri ambao utakwenda kuondoa changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo mwaka uliopita.

Alisema katika kutekeleza azma ya serikali, TCDC kwa kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa stakabadhi za ghala na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) imeandaa mwongozo wa biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala wa mwaka 2021 kwenye mazao ya choroko, soya, ufuta, mbaazi na dengu kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji wenye tija na kupata bei zenye ushindani.

“Mwongozo huu unaelekeza kila mkulima na wadau wengine watalipwa fedha zao zote kupitia akaunti benki ili kurahisisha malipo haya kufanyika kwa wakati, kila mkulima anatakiwa kuwa na akaunti yake , mfumo wa malipo kupitia akaunti ya benki ni salama kwa wakulima wetu na unaleta usalama wa fedha yenyewe kwa mkulima,” alisema.

Alisema malipo ya fedha za mauzo yatafanyika ndani ya siku tano za kazi kwa wakulima na wadau wengine baada ya mnunuzi kulipa na malipo hayo yanafanywa na mnunuzi kwenye akaunti ya soko la bidhaa Tanzania na fedha zitahamishwa kwenda kwenye akaunti ya chama kikuu cha ushirika ndani ya masaa 12.

Pia alisema mwongozo huo unatoa maelekezo mazao yote yanayozalishwa na wakulima yatakusanywa kwenye ghala la vyama vya ushirika na kusafirishwa kwenda kwenye ghala kuu (ghala la mnada) na taarifa zote za mazao zitapelekwa kwenye ghala kuu.

“Mazao yanayokusanywa kwenye vyama vya ushirika yatapelekwa ghala kuu ambapo taarifa za mazao yaliyopokelewa ghala kuu zitatumwa kwenye soko la bidhaa na kuuzwa kwa mnada kwa njia ya kielektroniki,” alisema.

Aliwataka viongozi wote ngazi ya mkoa hadi wilaya ambako mazao hayo yanalimwa kusimamia vizuri kazi hiyo ili kuhakikisha muongozo huo unatekelezwa kikamilifu katika maeneo yao.

Aidha alibainisha kuwa kwa mujibu wa muongozo huo mnunuzi lazima awe amesajiliwa na soko la bidhaa Tanzania ili aweze kushiriki katika minada ambayo itakuwa inafanyika kila wiki na usajili huo unafanyika kuanzia sasa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Soko la bidhaa Tanzania TMX.

Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani unawezesha soko la bidhaa Tanzania kusaidia wakulima kupitia vyama vya ushirika kuuza mazao yao katika soko la ushindani ambapo soko la bidha aTanzania linafanya minada ya wazi kwa njia ya kielektroniki.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani, Asangye Bangu alisema ukusanyaji wa bidhaa uzingatie sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuhakikisha sifa ya bidhaa zinazofikishwa ghalani zimekidhi vigezo na kuwa na ubora.

Mtendaji Mkuu wa Soko la bidhaa Tanzania (TMX) ,Godfrey Malekano alisema mbali na faida nyingine za mfumo huo ni kwa wanunuzi kuepuka gharama kwani mfanyabiashara wa Dodoma anaweza kushiriki mnada wa Simiyu kwa njia ya mtandao bila kwenda Simiyu kushiriki mnada.

Chanzo: habarileo.co.tz