Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Soko la hisa laongeza mtaji kampuni za ndani

Ddeb171af7914f88f3bc2932912a2f05.jpeg Soko la hisa laongeza mtaji kampuni za ndani

Sat, 25 Jun 2022 Chanzo: Habari leo

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limefanikiwa kuongeza mtaji wa kampuni za ndani kutoka Sh trilioni nne mpaka Sh trilioni 10 kwa upande wa hisa. Aidha, hatifungani, mtaji wa kampuni za ndani umeongezeka kutoka Sh trilioni tano hadi kufikia Sh trilioni 15.5.

Mafanikio hayo yamo katika taarifa mbalimbali za mauzo na manunuzi za miaka tisa kuanzia mwaka 2013. Uchambuzi uliofanywa na gazeti hili katika ripoti mbalimbali za DSE zinabainisha kwamba pamoja na kuwapo na ugonjwa wa Covid-19 uliovuruga uchumi wa dunia, bado DSE imepata maendeleo ya kutosha hasa ongezeko la ukwasi.

Ripoti za DSE zinaonesha ongezeko la ukwasi sokoni kutoka wastani wa Sh bilioni 50 mpaka kufikia wastani wa Sh bilioni 500 kwa mwaka kwa upande wa hisa na kutoka Sh bilioni 300 hadi kufikia Sh bilioni 2,500 kwa upande wa hatifungani. Vilevile wanahisa katika kampuni zilizoorodheshwa wameongezeka kutoka 250,000 hadi kufikia 600,000.

Taarifa zinaonesha pia kuwapo ongezeko la ufanisi na faida kwa kampuni ya DSE kutoka utengenezaji hasara hadi kufikia wastani wa faida ya Sh bilioni tano kwa mwaka. Kuhusu mtaji na mzania wa mahesabu ya kampuni ya DSE, ripoti zinaonesha kwamba zimeongezeka kutoka Sh bilioni tatu hadi kufikia Sh bilioni 25 kwa ukubwa wa mtaji na Sh bilioni 28 kwa ukubwa wa mzania wa mahesabu.

Mafanikio mengine yanayoonekana katika kipindi cha miaka hiyo tisa kwa kuzingatia ripoti mbalimbali ni kuanzishwa kwa utaratibu wa kukuza mitaji ya ujasiriamali, kubadili mifuko ya tehama ili kuleta mifumo yenye ufanisi kwa bei nafuu, kubadili mfuko wa kisheria na kiutendaji ili kuboresha na kuimarisha taratibu za utawala bora.

Chanzo: Habari leo