Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Soko kuu la dhahabu lazinduliwa Chato, Waziri Biteko atoa maagizo

90139 Dhahabu+pic Soko kuu la dhahabu lazinduliwa Chato, Waziri Biteko atoa maagizo

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chato. Wizara ya madini nchini Tanzania inakusudia kuingiza biashara ya madini kwenye mfumo wa kidigitali ili kuepuka utoroshwaji wa dhahabu kwenda nje ya nchi hiyo.

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 27,2019 wakati wa uzinduzi wa soko kuu la dhahabu Chato mkoani Geita lililojengwa eneo la Buseresere wilayani Chato mkoani Geita.

Amesema kuingia kwenye mfumo wa digitali kutamsaidia mchimbaji kufanya biashara kidigitali ambapo mchimbaji atatoa taarifa za kuuza dhahabu kwa kutumia ujumbe mfupi na kwamba ili liwezekane mialo yote lazima isajiliwe na kupewa namba.

Biteko ametaka shughuli ya kusajili mialo (eneo la kusafisha udongo unaosadikiwa kuwa na dhahabu) lifanyike kwa uadilifu na kuwataka wachimbaji na wafanyabiashara kuacha kuweka mialo kila eneo.

“Nia yetu ni moja, tunataka kujua dhahabu inayozalishwa imetoka wapi baada ya muda sio mrefu tunatengenea mfumo ambao mchimbaji hahitaji kutembea na makaratasi yeye atatuma tu meseji ambayo itamtambalisha akiwa popote akielekea sokoni atakua kwenye mfumo ambao yeye, ofisa madini na mtu wa wizara ndio watakua na taarifa,” amesema Biteko

Aidha ametoa siku saba kwa ofisi ya madini mkoani Geita kutoa leseni za uchenjuaji kwa wafanyabiashara wa madini zaidi ya 300  wenye mitambo ya kuchenjua dhahabu mkoani humo ambapo alisema wafanyabiashara kufanya kazi bila kuwa na leseni ni kuisababishia serikali hasara na haikubaliki.

Waziri Biteko amewataka wachimbaji kuachana na biashara ya kujionyesha kwa kupanga kreti za bia na kuwataka wachimbe kibiashara ,walipe kodi na wawekeze kwenye miradi ya kimaendeleo ili kuongeza kipato chao na jamii inayowazunguka

Akizungumzia uwepo wa masoko Geita, Biteko amesema kwa sasa yapo masoko 29 ya madini nchini huku nane kati ya hayo yakiwa mkoani Geita ambapo alisema uwepo wa masoko hayo umewezesha kuongeza mapato ya serikali kutoka Sh1 bilioni zilizokuwa zikizalishwa awali  na sasa Serikali inapata zaidi ya  Sh234 bilioni kwa mwezi.

Awali, Waziri wa nishati, Dk Merdad Kalemani ambaye pia ni mbunge wa Chato ameiomba wizara ya madini kutoa vibali kwa madalali wa  dhahabu ili waweze kusafirisha kwenda nje ya nchi tofauti na sasa vibali vyao ni vya ndani ya mkoa pekee.

Chanzo: mwananchi.co.tz