Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simulizi ya mama mlemavu aliyezawadiwa bajaj na Diamond

27549 MAMA+PIC TanzaniaWeb

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. 0ktoba 5, 2018 ni siku ambayo ilibadili maisha ya Evodia Nchimbi, mama mwenye ulemavu wa miguu ambaye anategemea magongo ili aweze kujongea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kwa kipindi cha miaka mitatu Evodia ambaye ni mama wa mtoto mmoja amekuwa akiendesha bajaj akitafuta hesabu ya mmiliki wa chombo hicho na kiasi kidogo kwa ajili ya familia yake.

Siku hiyo Evodia alimwaga machozi ya furaha baada ya ndoto yake ya muda mrefu ya kupata bajaj yake kutimia.

Mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye alimuona mama huyo akihojiwa Wasafi Tv na kuguswa na hali yake akaamua kumpatia bajaj hiyo ili aweze kuendesha maisha yake.

“Nilikuwa naendesha bajaj ya mkataba, ilipofika muda ambao nimemaliza mkataba wa bosi na tayari chombo kile kikawa mali yangu kuna siku nilikuwa natembea na magongo yangu bahati mbaya nikateleza,

“Kuteleza kule kulinifanya nivunjike mguu hivyo nikajikuta nimekaa nyumbani miezi mitatu nikijiuguza, nikaona ni bora nimpe mtu aendeshe ili niweze kupata hela ya kula muda wote nitakaokuwa nyumbani,

“Yule mtu alikuwa mwaminifu kila siku akawa ananiletea hela sasa pale Feri kuna kawaida ya kupeana deiwaka kama ilivyo kwenye magari, kuna siku mtu akamuomba naye bila hiyana akampa huwezi amini aliondoka nayo moja kwa moja,” anasema.

Licha ya kupata simanzi moyoni mwake Evodia hakukata tamaa alifanya upelelezi kujua ni wapi hasa mtu huyo alipokwenda na bajaj yake ndipo alipopata taarifa kwamba yuko Moshi.

Nikafunga safari hadi Moshi kwa msaada wa askari tukafanikiwa kufika kwenye kijiji ambacho alijificha mhusika, akakamatwa na kuhojiwa akasema na yeye aliibiwa Mwananyamala, polisi wakamuweka ndani na hatimaye akasafirishwa mpaka Dar es Salaam, malalamiko yangu yakahamishiwa kituo kikuu cha polisi,”

Anasema, “Ndugu wa mtuhumiwa huyo walifika polisi na kuomba niwape miezi sita watanilipa lakini askari mmoja akanishauri ni heri nikubali maana akishtakiwa atafungwa halafu nisipate chochote nikaona nikubaliane na hilo ndio nasubiri hiyo miezi sita inaishia Januari.”

Akizungumza huku akibubujikwa machozi anasema alikata tamaa ya maisha na kujiona mwenye mikosi hivyo alilazimika kuanza upya kutafuta bajaj ya mtu ili kupata chochote kwa ajili ya kuendesha familia yake.

Akiwa na bajaj hiyo ndipo alipokutana na vijana wa Wasafi Tv waliovutiwa naye kumfanyia mahojiano ambayo Diamond aliyaona na kuamua kumkabidhi zawadi ya bajaj ambayo imekuwa mali yake.

Alifikaje Tandale

Anasema alifika Uwanja wa Maguniani bila kufahamu kama atapata msaada huo kwani vijana wa Wasafi Tv walimwambia kwamba wanataka kuhitimisha mahojiano yao huku wakimsisitiza kuwa Diamond angekuwepo hivyo wanaweza kumuelezea shida zake.

“Siku hiyo mvua kubwa ilinyesha mjini roho yangu ikawa inasita mno kwenda kule lakini mmoja wao akanipigia na kunisisitiza nisikose, nikajisemea rohoni acha tu niende, nilipofika akanifuata na kunisaidia kunipandisha jukwaani na akaniambia hapa Diamond atatoa bima za afya na kumpa mama mmoja bajaj, ila wewe hautapewa kitu usijisikie vibaya itakuwa fursa nzuri ya kumuelezea matatizo yako.

“Kwa hiyo nilikaa pale sijui hili wala lile nikijua hakuna linalonihusu zaidi ya kusubiri kurekodiwa, nikashangaa ametangaza kwamba mimi ndiye mama ninayetakiwa kupewa bajaj, sikuamini na hadi leo nasema Mungu ambariki kuonyesha shukrani zangu bajaj aliyonipa nitaweka picha yake.”

Maisha yake

Kilio chake kwa sasa kinabaki kwenye mazingira anayoishi ambayo si salama kwa mtu mwenye ulemavu.

Mama huyu na binti yake wanaishi kwenye chumba kimoja walichopanga Mburahati kwenye nyumba ambayo ina wapangaji wengine na fremu za biashara.

Watu wote hao wanategemea choo kimoja ambacho kwa Evodia anaamini si salama kwake kutokana na hali ya ulemavu aliyonayo.“Ni lazima niwe na ndoo ya kukalia kule chooni, yaani kiukweli inanipa shida kwa sababu wakati mwingine najikuta nagusa chini na choo chenyewe si kisafi kiasi hicho. Hakina mlango wala kitasa basi ni changamoto kwa kweli.

Hamu yake kubwa ni kujenga nyumba angalau yenye vyumba viwili ambayo itamruhusu kuweka choo chake ndani atakachokitengeneza kwa kuzingatia mazingira ya mtu mwenye ulemavu.

“Naomba atokee mtu atakayeguswa na kunisaidia nikifikia angalau kupata kiwanja niko tayari kujenga hata nyumba ya tope ili tu niwe na choo changu ndani.”

Historia yake

Evodia alizaliwa miaka 35 iliyopita wilayani Peramiho, mkoani Ruvuma akiwa ni mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto sita. Alizaliwa akiwa mzima ila alipata ulemavu akiwa na miaka minne baada ya kuugua polio. Kwa jitihada za mama yake alimfikisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini hakupona zaidi ya kufanyiwa mazoezi ya viungo yaliyomuwezesha angalau kutembea kwa magongo.

Alisoma hadi darasa la saba na kisha kujifunza ushonaji wa nguo, kazi ambayo aliamini angeweza kuimudu kutokana na hali yake ya ulemavu.

Miaka miwili baadaye mama yake alifariki na kumuachia jukumu la kulea wadogo zake watano wakati akiwa na umri wa miaka 17.

Alifanya kazi hiyo kwa muda kabla ya kuamua kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta fursa zaidi. Bahati ikawa upande wake akapata kazi kwa fundi mmoja ambaye alikuwa akimlipa Sh5,000 kwa siku hivyo alikuwa akianza kushona asubuhi hadi jioni kwa ujira huo.



Chanzo: mwananchi.co.tz