Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku ya kahawa na umuhimu wake

Fb4867a8bd5d35dea652501835563e0a Siku ya kahawa na umuhimu wake

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KWA wengi, kikombe kimoja cha kahawa kinaweza kuifanya siku yao kuwa yenye kuchangamka zaidi na murua.

Wengine hutumia kinywaji cha kahawa kama njia ya kupitisha muda na kubadilishana mawazo hasa wanapokutana na marafiki zao.

Kila Oktoba mosi ya kila mwaka, hufanyika maadhimisho ya siku ya kahawa duniani ambayo hukutanisha wadau mbalimbali wa kahawa, bodi ya kahawa, wanunuzi, wazalishaji, wachakataji, waandaaji wa mbegu za mibuni na wakulima wa zao hilo.

Kwa mwaka huu, Mkoa wa Kagera uliadhimisha Siku ya Kahawa Duniani tarehe 10/10/2020 katika hafla iliyofanyika wilayni Muleba.

Muleba ilipata fursa ya kuandaa maadhimisho ya mwaka huu kwa sababu ndiko alikotokea mkulima bora wa kahawa kwa mwaka 2019/2020.

Katika msimu uliopita, 2018/2019, maadhimisho kama hayo yalifanyika wilayani Kyerwa ambako ndiko pia alikotokea mkulima bora katika msimu huo.

Ofisa Ubora wa Bodi ya Kahawa, Kanda ya Ziwa, Jimmy Mchau alitumia maadhimisho hayo kuwaeleza wakulima wa kahawa pia kunywa kahawa kutokana na manufaa yake mbalimbali.

Anasema faida zitokanazo na unywaji kahawa mbali na kuchangamsha mwili ni pamoja na kuyeyusha mafuta mwilini, kukabiliana na ugonjwa wa kisukari, kuzuia maradhi ya kupoteza kumbukumbu, kulinda afya ya ini na kuondoa msongo wa mawazo.

Anazitaja faida nyingine kuwa ni kahawa kuwa na virutubisho muhimu mbalimbali vya kulinda mwili wake kukabiliana na maradhi mbalimbali kama ya saratani, maradhi ya moyo kama kiharusi pamoja kuondoa magonjwa ya uzee, ikiwa ni pamoja na kumfanya mtu aishi umri mrefu.

Kwa hiyo, mbali na kuzalisha kahawa, msiachie watu wengine kunufaika nayo, na nyinyi mnywe kahawa kwa wingi ili kupata faida lukuki za kiafya, anasema.

Anasema mpaka sasa ni asilimia saba tu ya wananchi wanaokunywa kahawa nchini lakini lengo ni kupandisha idadi hiyo hadi angalau kufikia asilimia 25 ya unywaji wa kahawa inayozalishwa nchini na Watanzania wenyewe.

“Bodi imejitahidi kufanya mambo mengi hii ni pamoja na kuuza kahawa sokoni moja kwa moja na kuacha kuuza kahawa kwa njia ya mnada. Tunaendelea kuwasaidia wakulima wetu kupitia vyama vya ushirika kuendelea kujisajili katika kilimo endelevu.

Tumeendelea kufanikiwa kuvuna kahawa ya madaraja ya juu baada ya kuwaelimisha wakulima kuongeza umakini katika uvunaji na utunzaji wa kahawa ili kupata fedha nzuri,” anasema Mchau.

Hata hivyo, anasema kwa kipindi chote, Bodi ya Kahawa imeendelea kusimamia vizuri majukumu yake kama kuratibu majukumu shirikishi ya wadau wa kahawa, kuangalia mwenendo wa uzalishaji kahawa, kufanya utafiti, ugani, uendelezaji masoko, kusimamia ubora wa kahawa pamoja na kuangalia namna pembejeo za kuinua kilimo cha kahawa zinavyopatikana.

Pamoja na elimu ya kujua faida za kahawa na kazi za Bodi ya Kahawa iliyotolewa, wakulima, wananchi na wadau walipata fursa ya kuonja kahawa na kutambua aina bora za kahawa kupitia maadhimisho hayo ya Siku ya Kahawa Duniani.

Mkoa wa Kagera umekuwa ukiendelea na kunadi kahawa yake hasa kuifanya kahawa inayozalishwa kupata soko la watumiaji wa ndani.

Katika muktadha huo, hivi karibuni wakati wa maonesho ya kilimo maarufu kama Nanenane mkoani Kagera, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa, Kanda ya Kagera (TaCRI) ilizindua vyakula mbalimbali na vinywaji vyenye kutengenezwa kwa kutumia ladha ya kahawa.

Katika maonesho hayo ya Nanenane wananchi walipata fursa ya kuonja vyakula vyenye ladha ya kahawa ambavyo sasa vinapatikana katika migahawa na mahoteli mbalimbali mkoani Kagera.

Katika maonesho hayo vijana pia walipata mafunzo ya bure ya namna wanavyoweza kutengeneza ajira kupitia kuandaa juisi, keki na biskuti zenye ladha ya kahawa na kuuza maeneo mbalimbali.

Mtafiti mwandamizi kutoka kutoka TaCRI, Nyabisi Ng’homa alisema kupitia vyakula vilivyoongezewa ladha ya kahawa vitaongeza watumiaji wa kahawa nchini kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia aslimia 15 ifikapo 2023 na kwamba lengo ni kufikia asilimia 50 ya matumizi ya kahawa kwa watanzania.

Anasema tukifika huko, hakutakuwepo na kulialia juu ya soko la nje bali kahawa nyingi itauzwa ndani kwa bei nzuri na kuongezewa thamani kwa ajili ya kuichanganya katika vyakula mbalimbali.

Katika kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri, Café Africa ambalo ni shirika lisilo la kiserikali na mdau mkubwa wa kahawa lilisema liko mbioni kufungua maduka ya kahawa ambayo yatatumiwa na wananchi wa kawaida kupata kinywaji hicho na hivyo kuongeza soko la ndani.

Daniel Mwakalinga ambaye ni mratibu wa shirika hilo anasema licha ya kuboresha kilimo cha kahawa, shirika hilo limejikita pia katika kuelimisha wananchi juu ya kutumia kahawa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera hasa maeneo ya vijijini ambako ndiko wakulima walipo na wao ndio wazalishaji wakubwa lakini hawatumii kahawa.

Anasema kwa sasa shirika hilo limefanya mafunzo katika wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Bukoba vijijini na mjini pamoja na Muleba ambapo kila wilaya kuna vijana watano wakulima wa kahawa watakaosaidiwa kufungua vibanda vya kahawa kwa ajili ya wananchi kujipatia kahawa.

Aidha anasema kuwa wakulima 450 ambao wamepata mafunzo kwa ajili ya kuelimisha wakulima kilimo cha kisasa cha kahawa watatumika pia kuhamasisha unywaji wa kahawa na faida zake kiafya.

Ntaki Charles, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika ndiye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani akimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richald Ruyango.

Ntaki alitumia siku hiyo kuwataka wakulima wa kahawa kuachana na kilimo cha mazoea au kuchukulia kilimo cha kahawa kama kilimo cha kurithi, badala yake wachukulie kama zao linaloweza kuwainua kiuchumi na kuwapatia fedha nzuri.

Anasema wakulima wengi hawajishughulishi hata kuandaa mbolea ambayo inaweza kuongeza uzalishaji badala yake hujitokeza zaidi katika kulalamikia bei lakini asilimia kubwa haishughuliki wala kugusa mibuni ya kahawa.

Hivyo anasema jamii inapaswa kubadilika na kulima ikilenga kupata mazao bora ambayo ndio itayapeleka sokoni na kuwa kichocheo cha bei nzuri.

Anasema Muleba inahitaji kuongeza hamasa ya kufungua migahawa wa kahawa ili kuongeza soko la ndani kwa sababu hakuna sehemu yenye mgahawa unaomwezesha mwananchi kunywa kahawa na kwamba endapo mgahawa utakuwepo utachangia ongezeko la soko la ndani.

Alberth Katagira, mkulima wa Kyerwa aliyeibuka mshindi katika msimu iliopita wa 2018/2020 anasema kilichompa ushindi ni utunzaji bora wa shamba, kilimo bora chenye mpangilio na utumiaji wa mbolea isiyokuwa na kemikali.

Mengine yaliyomfikisha kwenye ushindi anasema ni uanikaji bora wa kahawa, uvunaji wa kahawa zenye viwango pamoja na utunzaji wa miche ya kahawa.

Anasema kila mkulima kama anaweza kuzingatia maagizo na maelekezo ya maofisa ugani anaweza kupata kahawa nyingi sana kwani kilimo chenye tija ni kile kinachozingatia kanuni bora za kilimo, ufatiliaji na uwekezaji.

Anasema wakulima wa kahawa mkoani Kagera wanaweza kufanya mapinduzi katika kilimo cha kahawa kama watawekeza nguvu, ufuatiliaji, matumizi ya mbolea isiyo na kemikali pamoja na kuachana na dhana ya mashamba ya kurithi badala yake wajikite katika kilimo cha kisasa.

Mkulima bora wa kahawa mkoani Kagera kwa msimu wa 2019/2020, Shakiru Kyetema, mkazi wa Muleba, anasema anatumia mashamba yake kuongeza thamani ya zao hilo kutoka katika kahawa ya maganda na kuifanya kuwa ya unga.

Anasema anauza kahawa yake nchini na nje ya nchi na hivyo amejipatia umaarufu mkubwa wa kahawa yake kukidhi viwango vya kununuliwa na watu wa chini kabisa kwani kahawa yake iliyo kwenye vifungashio bora inapatikana kuanzia shilingi 500.

Anasema ana mashamba bora ya kahawa huku akiendesha kilimo cha umwagiliaji na kutumia mbolea isiyokuwa na kemikali na kwamba kikubwa anahamasisha matumizi ya kahawa kama kinywaji chenye faida.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya sekta ya kahawa Tanzania iliyotolewa Aprili mwaka 2019 na Bodi ya Kahawa (TCB), watumiaji wakubwa wa kahawa ya Tanzania ni Japan asilimia 27, Ujerumani asilimia 17, Ubelgiji asilimia 12 na Italia asilimia 10.

Bodi hiyo ilitaja masoko mapya yanayotarajiwa kufikiwa kuwa ni India, Urusi, China, Australia na Afrika Kusini.

Chanzo: habarileo.co.tz