Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Siku 42 ngumu kwa taasisi, mashirika 129 ya serikali

88351 Pic+mashirika Siku 42 ngumu kwa taasisi, mashirika 129 ya serikali

Sat, 14 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Viongozi na wakurugenzi wa bodi za taasisi na mashirika 129 ya umma yatakayoshindwa kutoa gawio serikalini ndani ya siku 42 kuanzia jana, watakuwa wamekosa sifa za kuwa viongozi.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati akipokea gawio kutoka taasisi na mashirika 13 ambayo yalitoa jumla ya Sh4.285 bilioni.

Waziri Mpango alisema kwamba ikifika saa 6:00 usiku wa Januari 23 mwakani, bodi hizo zitakuwa zimevunjwa.

“Watendaji wakuu wa hizo taasisi nao hivyo hivyo sijui mimi nateuliwa na nani na nani, amri ndiyo hiyo. Hiyo ndiyo amri ya Serikali. Mchezo umekwisha, lazima Tanzania iende mbele,” alisema Waziri Mpango.

Agizo kama hilo lilitolewa Novemba 24 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na Rais John Magufuli wakati akipokea gawio la Sh1.05 trilioni lililotolewa na taasisi na mashirika 79 ya umma.

Rais Magufuli alitoa siku 60 kwa taasisi na mashirika 187 yaliyokuwa bado hayajawasilisha michango na gawio, kufanya hivyo.

Rais Magufuli alisema Serikali imewekeza mtaji wa Sh59.6 trilioni katika taasisi na mashirika 266, hata hivyo ameshangaa kuona ni mashirika 79 pekee ndiyo yametoa gawio kwa mwaka 2018/19, huku mashirika 187 yakishindwa kufanya hivyo.

“Baada ya siku 60, bodi za mashirika hayo 187 ambazo zita-kuwa hazijaleta gawio zijivunje zenyewe. Waziri, waandikie barua na kama ni wa kuteuliwa na mimi maana yake ikifika siku hiyo, kama ni mwenyekiti basi siyo mwenyekiti tena, kama wameteuliwa na mamlaka nyingine wazivunje hizo bodi,” aliagiza Rais Magufuli.

Katika mazungumzo yake jana, Waziri Mpango alisema watatoa fursa nyingine kwa makampuni, mashirika na taasisi kupeleka gawio na michango yao kabla ya muda huo alioutoa haujafika.

Alisema hadi kufikia jana jumla ya kampuni, mashirika na taasisi 58 kati ya 187 zilikuwa zimetoa gawio na michango yenye thamani ya Sh 12.12 bilioni.

“Natarajia mwaka kesho mtakuwa hapa tena,” alisema Waziri Mpango.

“Nitakuwa pembeni ya mheshimiwa Rais wakati anapokea gawio. Mlete zaidi kila mmoja wenu. Ni challenge (changamoto), msirudi tena kuleta hivi kidogo. Mmefanya vizuri lakini mfanye zaidi ili tufanye vizuri kwa ajili ya Watanzania masikini,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz